Breaking News: Babu Seya na Mwanaye Watinga Ikulu Kumshukuru Rais Magufuli kwa Kuwasamehe


Mwanamuziki Nguza Vicking “Babu Seya” na wanae Johnson Nguza “Papii Kocha”, Francis Nguza na Michael Nguza walipofika Ikulu jijini Dar Leo Januari 2, 2018 kumshukuru Rais Magufuli kwa msamaha wake aliotoa kwao dhidi ya kifungo cha maisha walichokuwa wakitumikia
Rais Dkt John Pombe Magufuli akiwa ameshikana Mikono na kuomba dua na Mwanamuziki Nguza Vicking “Babu Seya” na wanae Johnson Nguza “Papii Kocha”, Francis Nguza na Michael Nguza walipofika Ikulu jijini Dar Leo Januari 2, 2018 kumshukuru kwa msamaha wake aliotoa kwao dhidi ya kifungo cha maisha walichokuwa wakitumikia

Waziri Mkuu: Vijana Jitokezeni Mlime Korosho


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka vijana wanaioishi kwenye mikoa ambayo zao la korosho linastawi wachangamkie kilimo cha zao hilo kwa sababu lina fursa nyingi.

“Mahitaji ya korosho ni makubwa duniani, korosho zinatumika mahotelini na kwenye mikutano mikubwa, zinatumika kwenye ndege, kwa hiyo bei yake lazima iwe kubwa,” alisema.

Ametoa wito huo Jumapili, Desemba 31, 2017 wakati akizindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

Waziri Mkuu alisema anaamini kuwa kijana yoyote mwenye nguvu ya kufanya kazi hawezi kushindwa kulima zao hilo kwa sababu halihitaji uangalizi mkubwa. “Kijana yeyote anaweza kulima zao hili kwa sababu ekari moja ina miche 37 hadi 40. Kuna mtu atashindwa kuangalia miche 37 hadi ikue?” aliuliza.

Waziri Mkuu alisema kilimo cha korosho ni rahisi lakini pia kilimo cha korosho ni rafiki wa mazingira, kwani miti ikikua inatunza mazingira na inasaidia kuleta mvua. Alisema mbali ya mikoa inayolima korosho ya Lindi, Mtwara, Ruvuma Pwani na Tanga, kuna mikoa mingine ambayo udongo wake umepimwa na kubainika kuwa zao hilo linaweza kustawi bila shida.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dodoma, Kigoma, Njombe, Songwe na kuongeza kuwa mikoa ya Singida na Manyara iko mbioni kukamilisha uchunguzi wake.

“Leo tumeanza usambazaji wa miche ya bure hapa Ruangwa ambao najua utafuatiwa na wilaya nyingine hapa nchini. Nimeelezwa kwamba mche wenye kutoa mazao mengi ni wa kuanzia miaka mitatu hadi saba, kwa umri huu miche ya korosho inaweza kuchanganywa na mazao mengine kama ambavyo mtashauriwa na maafisa kilimo ili wakati wa palizi ya hayo mazao, shamba lako la korosho libakie kuwa safi,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa, yuko kwenye mapumziko ya mwisho wa mwaka jimboni kwake.

Mapema, akitoa taarifa ya taarifa ya uzalishaji wa miche ya mikorosho msimu wa 2017/18 mkoani Lindi, Katibu Tawala wa mkoa huo, Bw. Ramadhani Kaswa alimweleza Waziri Mkuu kwamba katika msimu wa 2016/2017, mkoa huo uliweka lengo la kuzalisha na kupanda miche 1,000,000 ya mikorosho.

“Hadi mwisho wa msimu huu, jumla miche 716,532 ilizalishwa na kusambazwa kwa wakulima sawa na asilimia 71.6 ya lengo lililowekwa. Kati ya hiyo, Halmashauri ya Kilwa ilizalisha miche 55,000, Halmashauri ya Lindi miche 100,000, Manispaa ya Lindi miche 50,000; Halmashauri ya Liwale miche 106,000; Halmashauri ya Nachingwea miche 227,670 na halmashauri ya Ruangwa miche 177,862,” alisema.

“Miche hii iligawanywa kwa wakulima bure ambao walipanda kwenye mashamba yao. Zoezi la tathmini ya miche iliyokua baada ya kupandwa linaendelea kwenye halmashauri zote za mkoa,” aliongeza.

Bw. Kaswa alisema kutofikiwa kwa lengo hilo kumechangiwa na kutopatikana kwa mahitaji yote ya mbegu na vifaa vya uzalishaji, kuchelewa kwa vifaa, na mwamko mdogo wa vikundi vya uzalishaji.

Alisema kwa msimu huu wa 2017/2018, mkoa uliweka lengo la kuzalisha miche ya mikorosho iliyobebeshwa na isiyobebeshwa 7,132,000. Kati ya hiyo, Wilaya ya Kilwa walilenga miche 1,122,000, Lindi Vijijini 1,550,000, manispaa ya Lindi 1,000,000, Liwale miche 450,000, Nachingwea miche 1,810,000 na Ruangwa miche 1,200,000.

“Hadi kufikia tarehe 29 Desemba, 2017 tayari miche 4,974,425 ilikuwa imezalishwa na iko tayari kwa kupandwa kwenye mamlaka za serikali za mitaa kama ifuatavyo:- Kilwa miche 772,000, Lindi Vijijini 1,160,455, manispaa ya Lindi 771,440, Liwale miche 266,000, Nachingwea 991,070 na halmashuri ya Ruangwa imezalisha miche 1,013,460,” alisema.

Sherehe hizo za uzinduzi wa upandaji miche mipya zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU

Mapato ya Korosho Mikoa Minne Yafikia Trilioni Moja


MAPATO kutokana na mauzo ya korosho katika msimu wa 2017/2018 katika mikoa minne ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma yamepanda na kufikia sh. trilioni 1.08 ikilinganishwa na misimu miwili iliyopita.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT), Bw. Hassan Jarufu alitoa taarifa hiyo Jumapili, Desemba 31, 2017 wakati akitoa ufafanuzi juu ya uzalishaji na mauzo ya zao la korosho nchini hadi kufikia mwisho wa mwaka 2017.

“Ukiangalia msimu wa mwaka 2015/2016, utaona kuwa korosho zilizozalishwa zilikuwa kidogo zaidi. Msimu huo ziliuzwa kilo 155,244,645 zikiwa na thamani ya sh. 388,474,530,906.00 ikilinganisha na msimu wa 2016/2017 ambapo jumla ya kilo 265,237,845.00 ziliuzwa zikiwa na thamani ya sh. 871,462,989,284.00,” alisema.

Alisema katika minada 10 ya msimu wa 2017/2018, mauzo ya korosho yamefikia kilo 285,828,205 zenye thamani ya sh. 1,082,200,383,581.00. “Mnada wa 10 ulikuwa tarehe 21 Desemba, 2017 na minada bado inaendelea kwa msimu wa 2017/2018,” alisema.

Akitoa ufafanuzi wa mauzo hayo kwa kila mikoa hadi kufikia mnada wa 10, Bw. Jarufu alisema Mkoa wa Mtwara umeongoza kwa kuuza tani 178,165.741 zenye thamani ya sh. 701,674,466,366.00 ukifuatiwa na mkoa wa Lindi ambao umeuza tani 68,687.504 zenye thamani ya sh. 247,163,294,296.00.

“Mkoa wa Ruvuma umeuza tani 19,545.613 zenye thamani ya sh. 76,173,400,063.00 na mkoa wa Pwani umeuza tani 19,429.347 zenye thamani ya sh. 57,189,224,856.00 na kufanya mapato yote kwa mwaka huu kufikia sh. trilioni 1.082,” alisema.

Bw. Jarufu alitoa ufafanuzi huo mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya upandaji mikorosho bora na mipya milioni 10 kwa msimu wa 2017/2018 mjini Ruangwa, mkoani Lindi. Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: “Korosho ni dhahabu ya kijani, tuitunze, itutunze”.

Bw. Jarufu alimweleza Waziri Mkuu kwamba Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele, Sekretarieti za Mikoa na Halmashauri za wilaya, imeendelea kutekeleza mpango wa miaka mitatu wa kupanda mikorosho 10,000,000 kila mwaka.

“Katika mpango huu, wastani wa mikorosho 5,000 inatarajiwa kupandwa katika kila kijiji au mikorosho 30 kwa kaya kwa mwaka, sawa na ekari 330,000 kwa mwaka kwa nchi mzima. Lengo la mpango huu ni kuongeza kiasi cha korosho kinachozalishwa nchini kwa kuongeza wigo wa halmashauri zinazozalisha korosho na kupanda miche inayotokana na mbegu bora zenye uzalishaji mkubwa na zenye ukinzani dhidi ya magonjwa na wadudu,” alisema.

Alisema katika msimu wa 2017/2018, Bodi ya korosho inaratibu uzalishaji wa jumla ya miche 14,001,820 ambayo imetokana na tani 100 (kilo100, 000) zilizozalishwa na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Naliendele.

“Mchanganuo wake ni kama ifuatavyo: kilo 31,170 za mbegu zitapandwa shambani moja kwa moja ambazo zitatoa jumla ya miche 2,181,900; kilo 68,830 zitazalisha jumla ya miche 11,819,920 kati ya miche hiyo isiyobebeshwa ni 9,636,200 na miche itakayobebeshwa ni 2,183,720.

“Ni matumaini yetu kuwa ifikapo mwishoni mwa mwezi Februari 2018, miche yote itakuwa tayari imezalishwa, kugawanywa na kupandwa katika mashamba ya wakulima,” aliongeza.

Mkurugenzi huyo alisema, katika msimu huu eneo la utekelezaji wa mradi limeongezeka kutoka Halmashauri 51 za msimu uliopita 2016/2017 hadi kufikia Halmashauri 90 nchi nzima  ikiwemo mikoa mipya iliyothibitishwa kustawi zao la korosho hapa nchini.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na wakuu wa mikoa ya Lindi, Mtwara, Ruvuma, Pwani na wajumbe wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT). Wakuu wa Wilaya, baadhi ya Wenyeviti wa Halmashauri na wataalamu kutoka kituo cha utafiti cha Naliendele walishiriki uzinduzi huo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Waziri Mkuu Atoa Kadi Za CHF Kwa Wazee 4,000


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kumudu gharama za matibabu bila kulazimika kuwa fedha taslimu.

Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Ruangwa na vijiji vya jirani katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CWT, mjini Ruangwa, mkoani Lindi.

“Leo hii nimetoa kadi za CHF kwa wazee 4,000 wa wilaya hii. Ninaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutenga fedha na kuwalipia wazee hawa ili wanufaike na bima hii ya afya kama ambavyo imeelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.”

“Ninatoa wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao; yaani mhusika, mwenza wake na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama huna fedha taslimu,” alisema.

Waziri Mkuu alikabidhi kadi kwa Mzee Issa Juma Ngalapa, mkazi wa kata ya Nachingwea pamoja na Mzee Suleiman Stola Lihepa wa kijiji cha Kilimahewa, kata ya Nachingwea kwa niaba ya wazee wote waliotakiwa kupatiwa kadi hizo.

Akitoa ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Andrea Chezue alisema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya kwa wazee wameuita ‘CHF Endelevu’ kwa sababu walifanya tathmini na kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, dawa zitaisha au wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.

“Katika Halmashauri tulifanya utambuzi wa wazee wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwenye vijiji vyote na kubaini kuwa kuna wazee 4,000. Tukaamua Halmashauri iwalipie sh. 15,000 kwa kila wazee sita kama ilivyo katika kaya ili tuweze kuchangia gharama za matibabu yao,” alisema.

“Mzee akipatiwa kadi hii, inakuwa ni ya kudumu, anaitumia miaka yote. Si ya kulipia kila mwaka kama zilivyo zile nyingine. Hadi sasa tumeshatoa kadi kwa wazee 2,700 na tunaendelea kutengeza kadi hadi tukamilishe zote. Tumepanga kuwa kila mwaka, tutafanya utambuzi wa wazee katika vijiji vyote ili wale wanaofikisha umri huo, nao pia waingizwe kwenye mpango huu,” alisema.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,

Polepole: Lema 2020 utalisikia hewani tu jimbo la Arusha Mjini


Katibu wa Itikadi na Uenezi  wa  Chama Cha Mapinduzi CCM, Humphrey Polepole amemtahadharisha Mbunge wa Arusha Mjini Godbless Lema kwakumwambia kuwa  kipindi hiki ni cha mwisho kuongoza Jimbo hilo la Arusha Mjini.

Hayo yamekuja mara baada ya Mbunge huyo kupitia kurasa zake za twitter kujibizana huku Lema akionyesha kumhoji Polepole kama familia yake huwa inamuelewa kweli anachokizungumza.

“Term ya mwisho Arusha, tunataka Mbunge wa Masuala na si wa Matukio, hata mkichezesha draft ili uende Hai, haitawezekana maana hata “fly to…” maji yako shingoni, na ukiamua kurudia kazi yako ya zamani. anko Siro is very serious,”ameandika Polepole

Habari Zilizopo Katika Magazeti ya Leo Jumanne ya January 2



Watu 120 wamekamatwa wakiwemo Mapadri nchini DRC Congo


Zaidi ya Makanisa 150 yaliandamana nchini DRC Congo December 31, 2017 wakimtaka Rais Joseph Kabila kuondoka madarakani katika maandamano hayo imetolewa taarifa na Msemaji wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Congo Florence Marchal

Katika taarifa iliyotolewa imesema watu saba wameuawa mjini Kinshasa na mmoja katika mkoa wa Kananga, katikati mwa Congo na kuongeza kuwa watu 82 wamekamatwa wakiwemo mapadri, katika mji mkuu Kinshasa, na 41 katika maeneo mengine ya nchi hiyo.

Katika hotuba yake ya kumaliza mwaka, Kabila amesisitiza kuwa kutangazwa  kwa ratiba ya uchaguzi wa December 2018, kumefungua njia ya maandalizi ya uchaguzi huo.