Mtanzania afungua mgahawa Sweden

TanzaniaIssa Kapande `Chef Issa.

Mgahawa mkubwa unaotoa huduma za chakula cha Kitanzania unaomilikiwa na mpishi maarufu duniani, Issa Kapande `Chef Issa', umefunguliwa nchini Sweden na kuvunja rekodi ya dunia.
Mgahawa huo ulizinduliwa na balozi wa Tanzania nchini Sweden, Mh. Dora Msechu.

Balozi Msechu alimpongeza Issa Kapande na mkewe kwa kufanikisha kuwapo kwa mgahawa huo ambao umeweka rekodi kuwa mgahawa mkubwa kuliko yote ya Kiafrika katika nchi za Ulaya.

Aidha, alimshukuru Torvald Brahm mwenyeji wa mji huo kwa kumuunga mkono Issa hadi kufanikisha ndoto yake ya kuwa na mgahawa wa kwanza wa Kiafrika katika mji wa Trollhattan utakatoa huduma ya chakula cha kitanzania.
Katika uzinduzi huo ambapo wenyeji wa manispaa hiyo akiwemo Meya na mwenyekiti wa Trollhattan, Paul Akerlund na msaidizi wake Peter Eriksson walikuwepo, balozi ambaye ndio kwanza ameanza kazi alielezea kufurahishwa na juhudi za Kapande.

Alisema Issa ameonesha njia kwamba inawezekana kwa watu waliopo Ughaibuni sio tu kuajiriwa, bali kujiajiri katika nyanja mbalimbali.Alisema hilo linawezekana kutokana na kufuatilia kwa karibu taratibu za wenyeji na kisha kutumia mafunzo yaliyopo kukamilisha ndoto.

"Ni dhahiri kuwa, Chef Issa kwa kupitia taaluma yake ya upishi amewezeshwa kumiliki mgahawa huu hapa Trollhattan,S weden kwa hilo, napenda tuishangilie na kuipigia makofi Sweden na Trollhattan."Alisema akimpongeza kijana huyo ambaye pia amewekeza mkoani Mtwara.

Katika mahojiano, Mpishi Mkuu Issa Kapande alisema mafanikio yake yanatokana na juhudi kubwa na nia aliyoiweka katika kujifunza na kufundisha wengine katika mitandao ya wapishi wakuu.
Alisema akiwa amefanyakazi katika nchi 17 na tayari akiwa na vitega uchumi nchini alianzia nia ya kuwekeza Sweden mwaka 2009 wakati alipohamia nchini humo akitokea Uswisi. Alisema alianza kwa kuomba vibali, lakini mchakato kamili ulianza mwaka 2013."Tulilazimika kufanya utafiti kidogo" alisema na kuongeza kuwa katika utafiti huo walihoji watu 300 na kujua mwelekeo hasa wa shughuli yao unastahili kuwaje.

Kapande ambaye ni mhitimu wa chuo kikuu cha Manchester Metropolitan na Chuo kikuu cha kimataifa cha menejimenti ya hoteli cha Uswis amesema amepambana vikali na mkewe hadi kufikia hatua ya kuanzisha mgahawa huo ambao upo katika eneo la ukubwa wa skwea mita 810.Kapande ambaye mwaka jana alitwaa tuzo ya dhahabu katika upishi akiwa na timu ya Sweden magharibi alisema kuna umuhimu mkubwa kwa wapishi wa nyumbani kukubali kubadilika na kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kujifunza na kufunza ili kuwa na aina nyingine ya mapishi katika kuendeleza sekta.

Ndani ya mgahawa huo pia watu mbalimbali watapatiwa taarifa za utalii Tanzania.
Katika kazi yake ya upishi, amebahatika kuwapikia watu mashuhuri duniani, baadhi wakiwa Andrew Young, Mchungaji Jesse Jackson, Robert Mugabe (Rais wa Zimbabwe), Paul Kagame (Rais wa Rwanda), Benjamini Mkapa (Rais mstaafu wa Tanzania), Raila Odinga (Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya), Daniel Arap Moi (Rais Mstaafu wa Kenya), Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Bi. Hillary Clinton na mumewe Bill Clinton, Mke wa Rais wa zamani wa Marekani Laura Bush.

Wengine ni Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein, mwigizaji Chris Tucker, Rais wa zamani wa Afrika Kusini hayati Mzee Nelson Mandela, Koffie Olomide, Youssour ndour, Arsene Wenger (Kocha wa Arsenal ya England), Gianluca Vialli (nyota wa zamani wa Italia aliyewahi kuichezea na kuinoa Chelsea ya England), Rais wa Congo DRC, Joseph Kabila, Billy Gates na wengine wengi.

Share on Google Plus

0 comments: