Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher ole Sendeka akisalimiana na Mganga Mkuu
wa Halmashauri ya Mji Njombe Dkt Samwel Ndalio Thomas mara baada ya
kuwasili Halmashauri hapo. Kulia kwake ni Mkuu wa Kitengo cha manunuzi
na mweka hazina wa Halmashauri.
Mhe. Ole sendeka akisalimiana na Karani wa Fedha “Cashier” wa Halmashauri Neema Kalundwa
Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Mji Njombe Illuminatha Mwenda akisoma taarifa ya
utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Halmashauri zilizofanyika.
Mhe. Ole
sendeka akionesha nakala ya kitabu cha Ilani ya uchaguzi ambapo
amewataka watumishi kuisoma na kila mmoja kuwajibika kwenye eneo lake
la utekelezaji kutekeleza ilani ya uchaguzi ya chama Cha
Mapinduzi.Kushoto kwake ni Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Jackson
Saitabahu akifuatiwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe Mhe. Ruth Msafiri.
Hyasinta Kissima –Njombe
Mkuu wa
Mkoa wa Njombe Mhe. Christopher Ole Sendeka amekutana na kufanya
mazungumzo na watumishi wa ofisi ya Mkurugenzi Halmashauri ya Mji Njombe
ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kujitambulisha mara baada ya kuteuliwa
kuwa Mkuu wa Mkoa huo.
Akiwasilisha
salamu za shukrani kwa mapokezi mazuri aliyopatiwa toka alipowasili
Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa, Mkoa wa Njombe ni miongoni mwa Mikoa
ambayo alipendelea sana kufanya kazi kutokana na uwepo wa fursa nzuri za
maendeleo, mandhari nzuri na hali nzuri ya hewa.
”Nimefurahi
sana kuwa katika Mkoa huu kwani kwa kipindi chote nilitamani sana
kufanya kazi katika MKoa wa Njombe na nilitamani sana kama nafasi hii
niliyoipata ningeipata kipindi nilipokua kijana lakini bado nafuraha
kubwa kwani ndoto yangu ya kuitumikia na kuifanya Njombe ya maendeleo
imeanza kutimia kupitia uteuzi wa Mhe. Rais na ninawahakikishia
kuwapatia ushirikiano wa kutosha katika yale yote mtakayoona yanahitaji
uwepo wangu.”alisema Mhe.Ole Sendeka.
Awali
akiwasilisha taarifa fupi ya utekelezaji wa shughuli mbalimbali za
Halmashauri mbele ya Mkuu wa Mkoa Mkurugenzi wa Halmashauri Illuminatha
Mwenda amesema kuwa, Halmashauri imejitahidi kufanya shughuli mbalimbali
za maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa zahanati katika kila kijiji,
ujenzi wa nyumba za waalimu katika shule mbalimbali za sekondari, utoaji
wa mikopo ya vijana na wanawake ambapo katika robo ya kwanza jumla ya
Tsh. milioni 52 zilitolewa kutoka mapato ya ndani huku shughuli za
ukusanyaji mapato mpaka kufikia sasa halmashauri imefikia asilimia 40%
ya ukusanyaji wa mapato kupitia mashine za ukusanyaji mapato(POS) 97
zilizopo katika maeneo yote ya ukusanyaji ushuru wa Halmashauri.
Mara
baada ya kuipokea taarifa hiyo Mkuu huyo wa Mkoa amesema kuwa kwa sasa
Chama Kilichopo Madarakani ni Chama Cha Mapinduzi chini ya Mhe. Rais
Dkt. John Pombe Magufuli, na hivyo watumishi wote hawana budi
kuhakikisha kuwa wanaipitia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi na kuhakikisha
kuwa kila mtu anasoma katika eneo lake na atambue kwamba ni kwa namna
gani anahusika katika utekelezaji wa ilani hiyo. Ameendelea kusema
hatakuwa na huruma kwa watendaji watakaoshindwa kukiri mapungufu na
kukubali kusahihishwa katika kutekeleza majukumu yao ipasavyo na yeye
hatakuwa na matatizo na mtumishi ambaye atatekeleza majukumu yake
ipasavyo na amewaonya wanasiasa wanaochochea migogoro na kukwamisha
shughuli za maendeleo kwani yeye hatakua na mswalia mtume kwa chama cha
aina yeyote ile.
“Mkurugenzi
Mhe. Rais amekuamini na amekuteua kuisimamia Halmashauri hii hakikisha
kuwa unasimamia watendaji wako wote mpaka wale watendaji wa ngazi za
chini Kabisa kama watendaji wa Vijiji, usiwaonee huruma kwani ukiwaonea
huruma wale wa juu hawatakuonea huruma wewe na mimi pia sitakuonea
huruma. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Halmashauri za Mkoa wetu zinakuwa
za mfano kwa kuwa na watendaji wenye weledi na wachapakazi kama kauli
ya Mhe. Rais inavyosema Hapa kazi tu.”ameendelea kusema.
“Naipongeza
Halmashauri kupitia taarifa yako Mkurugenzi kwa kuhakikisha kuwa kwa
vipindi vyote Halmashauri ya Mji Njombe haijawahi kupata mlipuko wa
ugonjwa wa kipindupindu na msibweteke kwa kulewa sifa hizo bali
hakikisheni Mji unaendelea kuwa msafi.
Mhe.
Sendeka ameiagiza Halmashauri kuhakikisha kuwa inatenga maeneo ya
upandaji miti kwa kadri halmashauri itakavyoshirikiana na wakala wa
barabara (TANROAD ) na idara ya misitu na mazingira ili kuhakikisha kuwa
wanapata aina nzuri ya miti itakayopandwa pembezoni mwa barabara za
watembea kwa miguu, maeneo ya taasisi na kila mwananchi ahamasishwe
kupanda mti nje ya eneo lake la makazi.
0 comments: