Wakati
katibu wa oganaizesheni wa CCM, Pereira Silima akikanusha kupitishwa
kwa sharti la ukazi kwa wagombea udiwani na ubunge, chama hicho
kimewataka watumishi wa umma walioshinda uchaguzi katika ngazi ya wilaya
kuamua moja; ajira au siasa.
Juzi,
katibu wa uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema katika kipindi cha
redio cha Times FM kuwa wanaogombea udiwani na ubunge mwaka 2020
watatakiwa kuwa wakazi wa maeneo wanayogombea, lakini mara moja akapata
maswali kutoka kwa wanachama.
Lakini
jana, Silima alisema CCM haiwezi kuweka sharti hilo kwa kuwa linakiuka
Ibara ya 67 (1 a-c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ambayo inaeleza
sifa za mtu ambaye hatakuwa na sifa za kugombea, hali kadhalika Sheria
za Uchaguzi.
“Nikiwa
katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa mwenye dhamana ya uchaguzi, napenda
kuwajulisha kwamba Chama cha Mapinduzi kimefanya mabadiliko katika
katiba yake,” anasema Silima.
“Mabadiliko
ambayo yamepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM Taifa uliofanyika
12/03/2017, pamoja na kanuni za uchaguzi wa chama na hakuna mahali
popote palipoandikwa kuwa wagombea wa udiwani na ubunge watajadiliwa kwa
sifa ya kuishi jimboni.”
Silima amewataka wanachama kuzipuuza habari hizo.
Katika
hatua nyingine, makamu mwenyekiti wa CCM, Phillip Mangula amewataka
watumishi waliogombea na kushinda nafasi za uenyekiti na ujumbe wa
wilaya, kuchagua moja; ajira au uongozi.
Katika
toleo la juzi la Uhuru, gazeti la chama hicho tawala, Mangula
amekaririwa akisema CCM itawashughulikia watendaji wake pamoja na watu
ambao walikiuka maelekezo ya waraka unaozuia watendaji wa Serikali
kuwania uongozi ndani ya chama.
Mangula
alisema baadhi ya wilaya na mikoa ilikiuka kwa makusudi waraka huo kwa
kutoa tafsiri potofu kama vile kueleza nafasi zilizozuiwa ni za
utendaji, jambo ambalo alidai si kweli.
Mangula
amekaririwa akisema waraka huo umeeleza bayana kwamba watumishi wa
Serikali hawaruhusiwi kuwania uongozi ndani ya chama. Alisema katika
hali ya kushangaza, baadhi ya watendaji kwa kushirikiana na wajumbe
wengine wa vikao vya uteuzi, wamewapitisha na wengine wameshinda nafasi
mbalimbali.
Alisema
CCM inaliona hilo kama tukio la uvunjaji wa kanuni za maadili ya
uongozi na hivyo inawataka wahusika kuanza kuwajibika kabla ya kusubiri
uamuzi wa vikao vya juu.
Mangula
alisema chama kinaweza kuchukua uamuzi wa kufuta matokeo ya uchaguzi
katika baadhi ya wilaya kitakapojiridhisha kwamba kulikuwa na ukiukwaji
wa kanuni kwa kuwa suala la rushwa ni kinyume na maadili ya viongozi wa
CCM.
0 comments: