Bodi
ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imesema baada ya
uchambuzi wa maombi ya mikopo ya elimu ya juu kwa mwaka wa masomo
2017/2018, orodha ya awamu ya kwanza yenye wanafunzi 10,196 wa mwaka wa
kwanza waliopangiwa mikopo imekamilika.
Mkurugenzi
Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru katika taarifa kwa umma
iliyotolewa leo Jumatano Oktoba 18,2017 amesema Sh34.6 bilioni
zimetengwa kwa ajili ya wanafunzi hao 10,196.
Amesema kwa jumla Sh108.8 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 30,000 wa mwaka wa kwanza kwa mwaka wa masomo 2017/2018.
Badru
amesema orodha ya awamu ya kwanza inapatikana kwenye tovuti ya Bodi ya
Mikopo http://www.heslb.go.tz/ na itatumwa kwa vyuo husika.
Amesema orodha nyingine (batches) zitafuata kwa kadri utaratibu wa udahili na uchambuzi unavyokamilika.
“Lengo
ni kutoa majina ya wote waliofanikiwa kupata mkopo kabla ya vyuo
kufunguliwa mwishoni mwa mwezi huu wa Oktoba, 2017,” amesema.
Mkurugenzi
mtendaji huyo amesema orodha hiyo ya wanafunzi 10,196 imepatikana baada
ya kupokea na kuchambua awamu ya kwanza ya majina ya wanafunzi 32,495
waliopata udahili katika chuo kimoja.
“Itakumbukwa
kuwa moja ya sifa kuu za kupata mkopo ni mwombaji kupata udahili katika
taasisi ya elimu ya juu inayotambuliwa na Serikali,” amesema.
Amesema
wanafunzi waliopata udahili katika chuo zaidi ya kimoja na ambao wana
sifa za kupata mikopo, watapangiwa mikopo baada ya kuchagua na
kuthibitisha chuo watakachojiunga kwa ajili ya masomo.
Wakati
huohuo, Badru amesema wanatarajia kuanza kutuma vyuoni fedha za mikopo
ya wanafunzi wanaoendelea na masomo ambao wamefaulu mitihani yao kuanzia
leo Jumatano, Oktoba 18, 2017.
Amesema Sh318.6 bilioni zitatolewa kwa wanafunzi 93,295 wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2017/2018.
“Tayari
Serikali imeshatoa fedha hizo na lengo la Bodi ni kuhakikisha zinafika
vyuoni kabla ya kufunguliwa kwa vyuo ili kuwaondolea wanafunzi
usumbufu,” amesema.
Bodi
imewasihi waombaji wa mikopo kuwa na subira wakati ikiendelea
kukamilisha maandalizi ya orodha zinazofuata za wanafunzi waliopata
mikopo.
0 comments: