Rais
John Magufuli akiagana na kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia duniani,
Prince Karim Al-Hussayni Aga Khan baada ya kufanya naye mazungumzo
alipomtembelea Ikulu, Dar es Salaam jana. (Picha na Ikulu).
***
RAIS
John Magufuli ametoa mwito kwa Taasisi za Aga Khan kupunguza gharama za
huduma zake kwa wananchi ili waweze kumudu, hasa ikizingatiwa kuwa
zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.
Rais
Magufuli alisema hayo jana alipokutana Ikulu Dar es Salaam na Kiongozi
wa Jumuiya ya Ismailia Duniani, Karim Aga Khan ambapo alimshukuru kwa
taasisi zake kutoa huduma za kijamii hapa nchini.
Pia
Rais Magufuli alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ipo tayari
kuendeleza na kuimarisha zaidi ushirikiano na Aga Khan na amemuomba
kiongozi huyo kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake, ikiwa ni
pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.
Akizungumza
na Rais, Aga Khan alisema Jumuiya ya Ismailia imedhamiria kuunga mkono
juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano kwa kupanua hospitali ya Aga Khan
iliyopo Dar es Salaam na kujenga chuo kikuu kikubwa katika Afrika
Mashariki mkoani Arusha.
Aga
Khan alisema kuwa upanuzi wa hospitali ya Aga Khan, utahusisha kuongeza
idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi kufikia vitanda
172, utaimarisha matibabu ya moyo, kansa na utaongeza ufundishaji wa
madaktari na wataalamu wengine wa afya.
Kuhusu
chuo kikuu kitakachojengwa Arusha, Aga Khan alisema Jumuiya hiyo
imedhamiria kujenga chuo kikuu kikubwa ambacho kitafundisha viongozi si
tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali pia Afrika nzima ili waweze
kuwa chachu ya mabadiliko na maendeleo ya Afrika.
Kwa
upande wa vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Aga Khan, alisema kuwa
yeye haamini kuwa yeye ni kipaumbele kwa vyombo vya habari kujikita
katika masuala ya siasa. Badala yake, alisema anaamini kuwa vyombo vya
habari vina wajibu mpana zaidi wa kujikita katika masuala ya maendeleo
hususani katika nchini zinazoendelea, na kwamba Aga Khan ipo katika
mchakato wa kujikita katika wajibu huo kwa kuwa na waandishi wa habari
na wachambuzi mahiri.
Wakati
huo huo, Rais Magufuli amekutana na kufanya mazungumzo na ujumbe wa
Maseneta wa Baraza la Seneti la Marekani, ambao ni wajumbe wa kamati ya
mazingira inayoshughulikia hifadhi ya taifa, wanyamapori na misitu ya
Marekani, ambao wamekuwepo hapa nchini kwa siku tatu kwa lengo la
kutembelea hifadhi ya taifa ya Ngorongoro.
Maseneta
hao ni James Inhofe, Mike Enzi, David Perdue, Luther Strange, Tim Scott
na John Thune. Baada ya mazungumzo hayo, Seneta James Inhofe na Seneta
Mike Enzi walimshukuru Rais Magufuli kwa kukutana nao na kuwakaribisha
wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Marekani kuja kuwekeza nchini.
Walikiri
kuwa Tanzania inazo rasilimali nyingi ambazo ni fursa muhimu ya kukuza
uchumi. Mazungumzo kati ya maseneta hao na Rais Magufuli, yalihudhuriwa
pia na Kaimu Balozi wa Marekani nchini, Dk Inmi Patterson.
Chanzo-Habarileo
Kazi kazi
ReplyDelete