Shinikizo la damu ambalo linaelezwa kuwa
kwenye kundi la magonjwa yasiyoambukiza na kuongoza kwa kusababisha
vifo kwa sasa, limemuua Sheikh wa Morogoro, Abdallah Mkang’ambe (48)
ikiwa ni miezi 17 tangu achaguliwe kushika wadhifa huo.
Akizungumzia kifo hicho, Msemaji wa
Jumuiya na Taasisi za Kiislam Tanzania, Rajabu Katimba alisema
wamepoteza kiongozi tegemeo na kipenzi cha watu na kwamba, atazikwa leo
Morogoro.
Akitoa taarifa za kifo hicho jana, Kaimu
Mwenyekiti wa Bakwata Morogoro, Sheikh Yahya Mrisho alisema Sheikh
Mkang’ambe alianza kuugua wiki iliyopita na kulazwa katika hospitali ya
rufaa Morogoro na baada ya hali yake kuwa mbaya alihamishiwa Hosptali ya
Taifa Muhimbili (MNH).
Hata hivyo, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano kwa Umma MNH, Aminiel Elgeisha alieza kuwa hakuwa na taarifa za kifo hicho.
Sheikh Mrisho alisema baada ya kifo
hicho, Bakwata makao makuu kwa kushirikiana na ofisi ya mufti walikuwa
wanafanya utaratibu wa kuusafirisha mwili kutoka Dar es Salaam hadi
Morogoro na kwamba, mipango ya mazishi inafanyika nyumbani kwake maeneo
ya Nanenane manispaa ya Morogoro.
Sheikh Mkang’ambe alichaguliwa Mei mwaka jana.
Watuma rambirambi
Sheikh wa mkoa wa Kagera, Haruna
Kichwabuta alisema ameguswa na taarifa za kifo hicho hasa ikizingatiwa
alikuwa kijana na tegemeo la Morogoro. “Tumempoteza kijana lakini ni
mapenzi ya Mungu tuendelee kumuombea,” alisema.
Naye Sheikh wa wilaya ya Morogoro,
Abdalrahman Kiswabi alisema kifo hicho kimeacha pengo kwa waislam na
Bwakata, kwani alikuwa ni kiungo na alipigania haki za waumini na
kudumisha amani.
Wengine walioguswa na kifo hicho ni
Padri Luitfrid Mkseyo ambaye ni Katibu mkuu wa jimbo Katoliki Morogoro
na katibu msaidizi wa kamati ya amani.
Padri Makseyo alisema kanisa hilo na
viongozi wa madhehebu mengine ya dini, limepata mshtuko kwa kuwa Sheikh
Mkang’ambe alikuwa kiongozi aliyehubiri amani na upendo wakati wote bila
ya kubagua dini. “Kwangu naweza kumzungumzia Sheikh Mkang’ambe kama
dira yetu viongozi wenzake hata waumini,” alisema.
0 comments: