Ujumbe wa watu zaidi ya 300 unaomwakilisha Mfalme wa Oman, Shekh Sultan
Qabous Bin Said umewasili visiwani Zanzibar leo Alhamisi asubuhi kwa
kutumia meli yenye jina la Fulk Al Salamah ambayo hutumiwa na mfalme
huyo.
Ujumbe huo wa Serikali ya Oman umewasili katika Bandari Kuu ya Malindi
mjini hapa majira ya saa tatu na nusu za asubuhi ikitokea nchini Oman.
Katika mapokezi ya ujumbe huo viongozi wa Serikali ya Zanzibar
walihudhuria akiwamo Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo,
Rashid Ali Juma, Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud
Mohamed, Waziri wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Salama Aboud Talib
na Wazir wa Biashara na Masoko, Amina Salum Ali.
Kwa upande wa ujumbe huo wa mfalme uliongozwa na Waziri wa Mafuta na
Gesi wa Oman, Mohamed Al-ramh ambapo lengo kuu la kufika Zanzibar ni
kusambaza amani na upendo ikiwa ni hatua ya kufikisha ulimwenguni kote.
Akizungumza katika mapokezi hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili
wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed amesema ni faraja kubwa kwa Zanzibar
kupata ugeni huo wa heshima.
Amesema ugeni huo ni ishara njema ya kufungua ukurasa mpya wa
ushirikiano baina ya nchi hizo mbili ambazo zinaonekana kuwa na udugu wa
kihistoria kwa miaka mingi.
‘’Ishara hii ni njema na tunaifurahia kwa moyo wote na kesho tutakuwa na
mazungumzo rasmi na ugeni huo ambapo tunataraji mambo mbalimbali
tutayajadili na baadaye kutoa taarifa rasmi ya mazungumzo yetu,” amesema
Aboud.
Hata hivyo amesema ujumbe huo pia utapa nafasi ya kutembelea maeneo
mbalimbali ya kihistoria, ofisi za Serikali lengo ni kubadilishana
mawazo juu ya ukuaji wa uchumi.
Waziri Aboud amewataka wananchi wa Zanzibar kuwapokea wageni hao katika maeneo tofauti ili kuonyesha ukarimu wao.
0 comments: