Wanandoa wawili Adam Charles Mtambo
41 na Mkewe Catalina Gabriel 39 wakazi wa Kitongoji cha Kasekese
B Kata ya Kasekese Wilaya ya Tanganyika Mkoa wa Katavi
wameuawa kikatili kwa kukatwa na mapanga na kushambuliwa kwa silaha
za jadi katika sehemu mbalimbali za mwili wao wakati wakiwa wamelala
pamoja kwenye kitandani kwao.Mwandishi wa Malunde1 blog,Walter Mguluchuma anaripoti.
Afisa Mtendaji wa Kata hiyo ya Kasekese Ramadhani Ibrahim alisema
kuwa tukio hilo la mauaji hayo ya kikatili limetokea usiku wa
kuamkia leo Jumamosi Oktoba 14,2017 majira ya saa saba kasorobo
nyumbani kwa wanandoa hao .
Alisema marehemu Adam ambae alikuwa ni mfanya biashara
anayemiliki maduka mawili Kijijini hapo, siku hiyo alifanya
biashara ya kuuza duka kama ilivyo kawaida yake na baada ya muda
wa kufunga duka ulipofika alifunga na waliingia ndani nyumba yao
kulala yeye na mke wake.
Alieleza kuwa wakati wakiwa wamelala ndani walitokea wauaji hao
ambao wanasadikiwa kuwa watatu na walifyatua risasi tatu za bunduki
hewani na kisha walivunja mlango na kuingia ndani ya chumba moja kwa
moja walichokuwa wamelala wanandoa hao.
Alisema baada ya kuingia chumbani waliwakuta wanandoa hao wamelala
kitandani na ndipo walipoanza kuwashambulia kwa kuwakata kata kwa
panga katika sehemu za usoni na kichwani na kuwashambulia kwa kutumia
silaha za jadi ikiwemo marungu na fimbo.
Asifa Mtendaji huyo wa kata alieleza kuwa marehemu alijaribu
kuwasihi waache kuwashambulia na aliwaeleza kuwa kama shida yao ni
fedha basi waache kuwakata kwa mapanga na kuwashambulia kwa silaha za
jadi na yeye yuko tayari kuwaonyesha mahali fedha zake zilipo
ili wasiendelee kuwashambulia.
Pamoja na kuwasihi hivyo wauaji hao waliendelea kuwashambulia tu kwa
mapanga hali ambayo iliwafanya marehemu na mkewe wazidi kupiga
mayowe ya kuomba msaada kwa majirani wao .
Alisema kutokana na mayowe hayo watoto wa marehemu ambao nao
walikuwa wakiishi kwenye nyumba hiyo wakiongozwa na kaka yao aitwaye
Charles waliingia chumbani kwa wazazi wao kwa lengo la kutoa
msaada.
Hata hivyo walishindwa kutoa msaada baada ya kushambuliwa na watu hao
kwa kuwapiga na marungu na fimbo hali ambayo iliwafanya wakimbilie
kwenye vyumba vyao vya kulala na kujifungia .
Majirani walifika kwenye eneo hilo na walikuta mlango wa mbele wa
nyumba hiyo ukiwa umevunjwa na walipoingia kwenye chumba walichokuwa
wanalala marehemu hao waliwakuta wakiwa wamelala chini ya kitanda huku
wakiwa na majeraha makubwa katika sehemu mbalimbali za mwili wao huku
damu zikiwa zimetapakaa kwenye chumba hicho .
Mwenyekiti wa Kitongoji cha Kasekese Happnes Bona alisema jitihada
za kutafuta usafiri kwa ajili ya kuwafirisha wanandoa hao kwa ajili
ya kuwapeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda zilifanyika na
hata hivyo wakati wakiwa njiani baada ya muda mfupi wanandoa hao
walifariki.
Alisema tangu amekuwa Mwenyekiti wa Kitongoji hicho hajawahi kuona
mauaji ya kutisha na y akikatili kiasi hicho kwani marehemu hao
waliuawa kwa kukatwa katwa kama wanyama na sio kama binadamu .
Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo miili ya marehemu hao imehifadhiwa
katika chumba cha kuhifadhi maiti katika hospitali ya Wilaya ya
Mpanda na baada ya uchunguzi wa kidaktari.
Katika hali inayotajwa kuwa huenda vifo hivyo vimetokana na visasi,wauaji hao hawakuondoka na kitu chochote baada ya kutekeleza mauaji hayo.
Jeshi la polisi mkoani Katavi limethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
0 comments: