Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema kimejipanga na kitampatia
mawakili wa chama Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe katika hatua yake ya
kumfungulia kesi ya kikatiba na ya madai Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam,
Paul Makonda.
Februari 8
mwaka huu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, alitaja majina 65
kwa tuhuma za kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya akiwamo Mbowe
na kuwataka kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam kwa ajili ya
kuhojiwa.
Lakini siku
moja baadaye Mbowe aliitisha mkutano na waandishi wa habari akiwa mjini
Dodoma ambapo alieleza kutofika polisi kwa wito wa Makonda akisema hana
mamlaka hiyo isipokuwa pale tu taratibu za kisheria zitakapofuatwa.
Mbowe ambaye
pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni aliweka bayana nia yake ya
kumfungulia mashtaka ya madai Makonda kwa kumkashifu na kumchafulia
jina.
Akitoa maazimio
ya kikao cha kamati ndogo ya Kamati Kuu ya Chadema jijini Dar es Salaam
jana, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Abdalah Safari alisema
kamati hiyo inaunga mkono hatua ya Mbowe kumfungulia kesi ya kikatiba
Makonda.
“Katika hili
tumejipanga kweli kweli…tutaungana na Mbowe katika kesi hii na
tutampatia mawakili wa chama akiwamo mimi na tuko wengi,”alisema.
Profesa Safari
aliwataka wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa kujihusisha
na biashara au utumiaji wa dawa za kulevya wafungue mashauri mahakamani.
“Tunatoa
wito kwa wale wengine wote ambao walitajwa na wanaamini kuwa walionewa,
kuchafuliwa majina na au kudhalilishwa wafungue mashauri mahakamani,
kwani hii ndio njia pekee ya kuzuia wengine wasifanyiwe uonevu kama huu
siku zijazo,”alisema Profesa Safari.
Pamoja na mambo
mengine, Profesa Safari alisema tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu 2015
viongozi na wanachama wa Chadema wamekuwa wakikamatwa na kushtakiwa kwa
makosa ya kubambikiziwa kwa kisingizio cha uchochezi.
Alisema mpaka sasa jumla ya wanachama na viongozi 215 wamefunguliwa kesi zaidi ya 78 nchi nzima.
“Kati ya hao
wengi wao wamenyimwa dhamana bila sababu za msingi huku wale ambao
walipatikana na hatia walipewa adhabu za vifungo bila kupewa fursa ya
faini.
“Kutokana na
hilo, hivi sasa tunaandaa orodha kamili itakayoainisha kesi zote za
jinai ambazo ziko mahakamani na kuonyesha aina ya mashtaka na vifungo
vilivyotolewa ambayo itawekwa wazi kwa vyombo vya habari na taasisi za
ndani na nje ya nchi kuthibitisha kuwa kuna mpango wa kuwafunga viongozi
wa upinzani kwa kusudi ili kuwadhoofisha,”alisema Profesa Safari.
Katika hatua
nyingine Profesa Safari aliwaomba marais wastaafu, mawaziri wakuu
wastaafu na majaji wastaafu kuzungumza na Rais John Magufuli kutokana na
yanayoendelea na kwamba wasiogope kwani wao hawatatumbuliwa.
“Marais
wastaafu Ali Hassani Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete wanaogopa
nini? Kwanini wasimwambie Rais Magufuli kuwa na wao waliapa kuilinda
Katiba ya nchi hivyo na yeye afanye hivyo.
0 comments: