Wafuasi wa Steven Wassira Waendelea Kumng'ang'ania Ester Bulaya....
Wapigakura
wanne wa Jimbo la Bunda waliofungua shauri kupinga matokeo ya Uchaguzi
Mkuu uliopita wameendelea kumng’ang’ania mbunge wa jimbo hilo, Ester
Bulaya kwa kukata rufaa kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu wa kutupa maombi
yao.
Msajili wa
Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, Francis Kabwe alisema jana kuwa rufaa ya
wapigakura hao, Magambo Masato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Acetic
Malagila iliyosajiliwa kwa namba 199 ya mwaka 2016, itasikilizwa
mfululizo kuanzia Februari 20.
Alisema rufaa
hiyo itasikilizwa jijini Mwanza na jopo la majaji watatu wa Mahakama ya
Rufani, Salim Mbarouk, Augustine Mwarija na Shabani Lila.
Katika maombi
ya msingi waliyofungua Mahakama Kuu, wapigakura hao wanaowakilishwa na
Wakili Constantine Mutalemwa, wanaiomba Mahakama kutengua ushindi wa
Bulaya dhidi ya aliyekuwa mgombea wa CCM, Stephen Wasira kwa madai kuwa
uchaguzi wa Oktoba 25, mwaka 2015 haukuwa huru na wa haki.
Pamoja na madai
mengine, Masato na wenzake wanadai kuwa mchakato wa kampeni, upigaji
kura na utangazaji wa matokeo uligubikwa na ukiukwaji wa sheria na
utaratibu wa uchaguzi, vikiwamo vitendo vya rushwa, msimamizi wa
uchaguzi kumnyima haki Wasira kwa kukataa ombi lake la kura kuhesabiwa
upya.
Hoja nyingine
ni msimamizi wa uchaguzi kutangaza matokeo bila Wasira kuwapo ukumbini
na kuchanganya tarakimu za idadi ya wapigakura walioshiriki uchaguzi.
0 comments: