Shangazi yake Mbunge wa Singida Mashariki
Tundu Lissu, Ninaa Sawa(kushoto) akiwa na mama mdogo wa Lissu, Bula Muro
nyumbani kwa wazazi wa Mbunge huyo Mahambe, Ikungi Singida. Picha zote
na Herieth Makwetta.
Siku 10 baada ya Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu
kushambuliwa na kujeruhiwa kwa risasi, familia yake imezungumzia tukio
na kusema mwishoni mwa mwezi huu watafanya kikao Dar es Salaam wajue
nini cha kufanya.
Baba mdogo wa Lissu, Muro Sawa (79), alisema kitu ambacho wazazi
wangefurahia ni kumwona kijana wao akirudi nyumbani akiwa mzima.
“Familia tutakaa kikao kushauriana ili tujue suala hili tunalitatua
vipi, lakini niiombe Serikali kumzidishia ulinzi kijana wangu. Sisi
familia tuna uchungu mkubwa kuhusu hili,” alisema Sawa.
Shangazi wa Lissu, Ninaa Sawa Muro (83) alisema, “Tunakula chakula
hakishuki, matonge yanakaba shingoni, maungo yote yanauma kwa sababu ya
mtoto wetu, tangu siku ile niliposikia nilikuwa kwenye kiti ghafla
nikaanguka na kuanza kutetemeka.”
Alisema alijisikia vibaya baada ya kuambiwa na mtoto wake taarifa hizo,
“Aliniuliza umesikia kwamba Tundu Lissu amepigwa risasi? Nikanyamaza,
nikaona joto. Kwa jinsi shangazi yangu anavyonipenda hata anikute
Manyoni hata Dar es Salaam ananiita jina langu la kikwetu anakuja
ananikumbatia iliniuma sana.”
“Alifanywa hivyo kwa nini? Kama tunavyojiona wote roho moja tumfikirie
huyo Tundu Lissu,” alisema shangazi huyo ambaye baada ya baba yake Lissu
kuzaliwa ndiye aliyemfuata.
Mama mdogo wa Lissu, Bula Muro, alisema baada ya kupata taarifa alianguka chini na kuanza kulia hakufikiria kama amepona.
Mitandao ilivyoiliza familia
Mmoja wa wanafamilia, Msengi Ntandu Mughwai alisema walipata shida siku
hiyo ya tukio, “Tulipanga kwenda Dodoma wakasema turudi anaendelea na
matibabu, tulihisi wanatudanganya sababu mtandaoni wanasema hali mbaya
na kwa kuwa walikuwa ni wanafamilia waliotushauri, tuliamua kurudi usiku
kwa kweli kesho yake kulikuwa na habari za ajabu kwenye mitandao yaani
zilituumiza sana,” alisema.
Msengi alisema walikuwa wakipigiwa simu na kupewa taarifa zenye utata na
wakiingia mitandaoni wanaona habari za ajabuajabu na kwamba hali kwao
ilikuwa mbaya.
“Kwa kweli tulipata shida, wazazi wetu walikuwa wanakuja mara kwa mara
tunawajibu kwamba anaendelea vizuri lakini wazee wetu walikuwa wanapata
taarifa mbaya kwingine kutokana na mitandao ya kijamii,” alisema.
0 comments: