Mwanamke aliyefahamika
kwa jina la Maria Mwanahiya mkazi wa kijiji cha Ntatumbila wilaya Nkasi
mkoani Rukwa amemjeruhi vibaya
mume wake kwa kumchoma kisu ubavuni kwa madai kuwa alipata hasira baada ya
kukerwa na kitendo cha mume wake kumlazimisha kuacha starehe zake ikiwemo
kunywa pombe.
Tukio hilo limetokea jana majira ya saa 10:30 usiku katika kijiji
cha Ntatumbila wilaya Nkasi mkoani Rukwa muda mfupi baada ya
mwanamke huyo kurejea nyumbani kutoka kilabuni alipokuwa anakunywa pombe.
Inaelezwa kuwa mwanaume huyo aliporudi nyumbani kwake kutoka katika
shughuli zake hakumkuta mke wake na wala mke hakuweka chakula kwa ajili ya mmewe
hali iliyomlazimu kumfuata mkewe kwenye kilabu ya pombe.
Alipofika
kilabuni, alimlazimsha mkewe kurudi nyumbani lakini mwanamke huyo
aligoma,hata hivyo baadhi ya watu waliokuwa wanakunywa naye pombe
walimsihi arudi nyumbani, ndipo alipokubali kwa shingo upande akarudi na
mmewe.
Baada ya kufika nyumbani ulizuka ugomvi mkubwa wa kurushiana
maneno kati ya wanandoa hao ambapo mwanamke huyo alikuwa akimwambia mumewe aache kumfuata fuata
anapokuwa kwenye starehe zake kwani yeye siyo mtumishi wa nyumbani.
Wakati wakiendelea kufokezana kwa muda mrefu, ndipo mwanamke huyo alipoamua
kwenda jikoni kuchukua kisu na kumchoma mumewe ubavuni na kumsababishia jeraha
kubwa ambalo lilivuja damu nyingi.
Tukio hilo lilisababisha watu kujazana katika nyumba
yao na kuamua kumkamata mwanamke huyo na kumpeleka kituo cha polisi
na mume wake kumkimbiza hospitalini ili akapatiwe matibabu ili kuokoa
maisha yake.
Afisa mtendaji wa kijiji cha Ntatumbila Daniel Kalumbilo ameiambia Malunde1 blog kuwa
hilo ni tukio la pili kwa mwanamke huyo kumshambulia mumewe kwa
silaha za jadi ambapo aliwahi kumpiga mpini na kumuumiza kichwa mpaka akafanyiwa
upasuaji.
Kamanda wa polisi mkoa wa Rukwa George Kyando amethibitisha
kutokea kwa tukio hilo na kuwasihi wanandoa kujitahidi kutatua migogoro yao kwa
njia ya amani na iwapo wanashindwa wawashirikishe ndugu wengine kuliko kupigana
na kuumizana.
0 comments: