Kamanda wa polisi Arusha Charles Mkumbo amewataka viongozi waliopo
karibu na kambi za mazoezi ya kijeshi kuweka utaratibu wa kuwakumbusha
wananchi kutoa taarifa pindi wanapoona vitu wasivyovijua hasa vyenye
asili ya chuma ili kuepusha madhara.
Kamanda Mkumbo ametoa hadhari hiyo alipokuwa akizungumzia tukio la vifo
vya watoto watatu wakazi wa kata ya Loksale wilayani Monduli
vilivyosababishwa na mlipuko wa bomu walilookota wakati wanachunga
mifugo na kuanza kulichezea kama mpira ambalo lililipuka na kuwajeruhi
vibaya miguuni.
Akizungumza kwa njia ya simu kamanda Mkumbo amesema licha ya kuwa tukio
hilo ni la bahati mbaya lakini lingeweza kuepukika kama watoto hao
wangeweza kutoa taarifa ya kitu walichokiona.
Kamanda Mkumbo amesema kuwa watoto hao wangeweza kufanya hivyo kama
wangekuwa wanakumbushwa na wazazi wao mara kwa mara wanapokwenda
machungani.
Kwa upande wa Mkuu wa wilaya ya Monduli Bw. Iddy Kimanta aliyezungumza
na ITV kwa njia ya Simu amesema watoto hao wote ni wanafunzi wa shule ya
msingi Nafko na wawili akiwemo Landisi Setabau miaka 12 na Samweli
Nyandusi miaka 9 walikuwa wanasoma darasa la kwanza wakati mwingine
aliyetajwa kwa jina la Seuri Losila miaka alikuwa darasa la tatu.
Viongozi wa eneo lililopotokea tukio hilo wamesema kimsingi tukio hilo
ni bahati mbaya kwani kwa muda mrefu wananchi wamekuwa wakielimishwa juu
ya kufuata maelekezo na mara nyingi wamekuwa wakitoa ushirikiano ikiwa
ni pamoja kutoa taarifa wanapoona mabaki ya vyuma.
Kwa mujibu wa viongozi hao katika maeneo mengi ya wafugaji wakati wa
likizo watoto huwasaidia wazazi wao kuchunga mifugo na pia wakati wote
wamekuwa wakitoa taarifa wanapokutana na vitu kama hivyo na wahusika
wamekuwa wakifika mara moja na kuvichukua.
0 comments: