WANAFUNZI 16,000 HATARINI KUKOSA MIKOPO ELIMU YA JUU 2017/2018
Wanafunzi wa elimu ya juu wapatao 16,000 kati ya 61,000 walioomba kupata
mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) wako
hatarini kuikosa hata kabla ya zoezi hilo kuanza kutokana na taarifa za
maombi yao kuwa na dosari.
Hata hivyo, uongozi wa juu wa bodi hiyo umesema wanafunzi hao bado wana
nafasi ya kurekebisha taarifa zao licha ya dirisha la kutuma maombi
kufungwa Jumatatu iliyopita.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul–Razaq Badru, akizungumza na Nipashe
kwa simu jana, alisema hadi siku ya mwisho ya maombi Septemba 11,
wanafunzi wanaokadiriwa kuwa 61,000 walikuwa wametuma maombi ya kupewa
mkopo kutoka bodi hiyo kwa mwaka ujao wa masomo 2017/18 utakaoanza
Novemba.
Alisema kati yao, wanafunzi 16,000 walikuwa na dosari ndogondogo
zilizoonekana katika maombi yao, huku wanafunzi wapatao 45,000 wakiwa
wamekamilisha vizuri taarifa za maombi hayo.
"Wanafunzi hao bado wanaruhusiwa kurekebisha taarifa zao kwa sababu
maombi hufanyika katika mtandao. Bodi bado inafanya uchambuzi wa
taarifa," alisema Badru.
Mkurugenzi huyo alizitaja dosari ambazo zimeonekana kwa wanafunzi wengi
waliotuma maombi ya mkopo kuwa ni pamoja na kutokuambatanisha vyeti,
kuambatanisha cheti ambacho hakijahakikiwa, baadhi ya barua za vyeti vya
kifo kutohakikiwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).
Alisema bodi hiyo bado inaendelea na uchambuzi wa taarifa za wanafunzi
hadi Oktoba 2 utakapokamilika na majina ya waliopangiwa vyuo yatakuwa
yameshatolewa.
Badru alisema wanafunzi ambao fomu zao zimebainika kuwa na matatizo,
hutumiwa ujumbe mfupi wa maneno (sms) na kutakiwa kurekebisha.
Aliongeza kuwa Oktoba 10 majina ya wanafunzi waliopangiwa mikopo yatakuwa yameshafahamika.
Jumuiya ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (Tahliso), kupitia kwa Mwenyekiti
wake, Stanslaus Kadugalize, ilitoa ombi jana kwa HESLB kutoa nafasi kwa
wale wote waliokosea kujaza fomu hizo, ili wafanye marekebisho
yanayotakiwa.
"Inawezekana waliojaza vibaya fomu hizo wanatoka katika mazingira magumu
ya maisha kiasi cha kushindwa hata kumudu matumizi ya kimtandao,"
alisema.
"Ili kuepuka kuwaacha walengwa, Tahliso tunaiomba Heslb iliangalie suala
hilo kwa jicho la pili, ili kuwapa nafasi kwa mara nyingine."
Alisema kuna uwezekano mkubwa wanafunzi waliokosea kujaza fomu hizo ndio
wenye uhitaji mkubwa kuliko waliopatia ujazaji wa fomu hizo.
WENGI WATAKOSA
Mei 13, akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na
Maendeleo ya Jamii, mjumbe wa kamati hiyo, Hussein Bashe, aliliambia
Bunge wamebaini wanafunzi wengi watakosa mkopo wa elimu ya juu katika
mwaka wa masomo 2017/18 licha ya kuwa na ufaulu mzuri.
Alisema mwaka jana (2016/17), wanafunzi 48,502 walijaza fomu kwa
ukamilifu, lakini 25,555 tu ndiyo walipata mikopo na hivyo kuacha
wengine 22,947 wakiwa hawana mikopo kutokana na bajeti iliyotengwa ya
Sh. bilioni 427.5 kutotosheleza mahitaji.
Bashe ambaye pia ni Mbunge wa Nzega Mjini (CCM), alisema mwaka 2017/18,
HESLB imeombewa bajeti ya Sh. bilioni 427.5 kwa ajili ya mikopo ya
wanafunzi (sawa na bajeti ya mwaka 2016/17) ilhali ufaulu wa wanafunzi
waliohitimu kidato cha sita umeongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2012
hadi asilimia 99 mwaka huu.
"Kamati inaona kwamba, suala la elimu ya juu ni haki ya msingi kwa watu
wenye sifa," Bashe alisema, "katika mwaka ujao wa fedha, wanafunzi wengi
zaidi watakosa mikopo licha ya ufaulu wao mzuri.
"Kamati inashauri serikali kuongeza bajeti ya HESLB, ili wanafunzi wengi
zaidi wanaostahili waweze kupata mikopo kwa maendeleo ya taifa letu."
0 comments: