
MTU na mkewe wameuawa kwa mapanga wakiwa
wamelala nyumbani kwao kwa kinachodaiwa walikuwa na kesi mbili za
kugombea ardhi Baraza la Ardhi la kata ya Hunyari, Tarafa ya Chamriho,
Bunda, Mara.
Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia
Oktoba 22, mwaka huu, katika kijiji cha Mariwanda, Hunyari. Ofisa tarafa
ya Chamriho, Boniphace Maiga jana alithibitisha na kuwataja waliouawa
kuwa ni Magina Masengwa (61) na mkewe, Sumaye Sebojimu (58) wa kitongoji
cha Kiborogota kijiji cha Mariwanda.
Maiga alisema wanafamilia hao walivamiwa
usiku nyumbani kwao wamelala na kukatwa mapanga na watu wanaodaiwa
walikuwa wameshitakiwa Baraza la Ardhi la Kata kuhusu kesi za migogoro
ya ardhi.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo
watuhumiwa walitoweka na kuziacha maiti za watu hao ndani ya nyumba hiyo
na kesho yake asubuhi mjukuu wao aliyekuwa anakwenda shambani alifika
nyumbani hapo kwa ajili ya kuwasalimia na ndipo alikuta wamekwishauawa
na kutoa taarifa kwa mamlaka husika.
0 comments: