Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
amemtumia salamu za rambirambi Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC)
Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa kufuatia kifo cha Askofu wa Jimbo
Katoliki la Tunduru Masasi Mhashamu Castory Msemwa, kilichotokea tarehe
19 Oktoba, 2017 nchini Oman.
Mhashamu Askofu Castory Msemwa amefariki dunia Mjini Muscat akiwa safarini kuelekea nchini India kwa Matibabu.
"Nimepokea
kwa masikitiko taarifa za kifo cha Baba Askofu Msemwa, kilichotokea
huko Oman, Baba Askofu Msemwa ametoa mchango mkubwa sio tu katika
kutimiza majukumu yake ya huduma za kiroho bali pia katika kuisaidia
jamii kupata huduma mbalimbali anazostahili binadamu na amekuwa akitoa
ushirikiano mkubwa kwa taasisi nyingine zikiwemo za Serikali katika
kudumisha amani, upendo, umoja na kuwahudumia wananchi, mchango wake
utakumbukwa daima" Amesema Mhe. Rais Magufuli.
Mhe.
Rais Magufuli amemuomba Rais wa TEC Mhashamu Tercisius Ngalalekumtwa
kumfikishia pole nyingi kwa Maaskofu wote wa TEC, Mapadre, Makatekista
na waumini wote wa Jimbo Katoliki la Tunduru Masasi kwa msiba huu mkubwa
uliotokea na amesema anaungana nao katika kipindi cha majonzi na maombi
kwa Marehemu.
"Raha
ya milele umpe ee Bwana na mwanga wa milele umuangazie, Marehemu Askofu
Castory Msemwa apumzike kwa amani, Amina" Amemalizia Mhe. Rais
Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
0 comments: