Wanachama wanaotaka kugombea ubunge kwa tiketi ya CCM, sasa watalazimika
kuwa wakazi wa eneo wanalotaka kuliwakilisha, sharti ambalo linaweza
kuwaondoa takriban nusu ya wabunge wa sasa.
Kutokana na Katiba ya Jamhuri ya Muungano kuruhusu mtu kwenda sehemu
yoyote apendayo, imekuwa rahisi kwa mtu kuishi mji kama Dar es Salaam na
kugombea ubunge wa jimbo lililoko katika mkoa mwingine.
Na uhuru huo umewawezesha watu kama Augustine Mrema, ambaye ni
mwenyekiti wa chama cha TLP, kuwa mbunge wa Moshi Vijijini kwa tiketi ya
CCM, Temeke (NCCR-Mageuzi) na Vunjo (TLP).
Na ni kutokana na uhuru huo, wabunge wengi wa vyama tofauti, wanaishi
Dar es Salaam na kuwakilisha majimbo ya maeneo ya asili yao.
Hata wafanyakazi kutoka serikalini, hasa wakuu wa mikoa na wilaya na
sehemu nyingine, huchukua likizo wakati wa uteuzi wa wagombea na kwenda
maeneo yao asilia au waliyokulia kuomba wapitishwe na wasipopitishwa
hurejea makazini.
Lakini masharti mapya ya CCM yanazuia mwanachama kugombea ubunge,
udiwani au nafasi nyingine yoyote bila ya kuwa mkazi wa eneo hilo.
“Shika maneno yangu, mwaka 2020 wagombea ubunge watakuwa ni wale ambao
wanatoka kwenye maeneo husika, wanaojua na kushughulika na shida za
wananchi,” alisema katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Humphrey Polepole
katika mahojiano na kituo cha redio cha Times FM jana.
Alisema hatua hiyo imetokana na chama hicho kujitathmini na
kujisahihisha baada ya kugundua watu wanataka viongozi wanaotoka
miongoni mwao ambao wanajua kero zao na hivyo wataweza kuzishughulikia.
Polepole, ambaye alipata umaarufu wakati wa Bunge la Katiba akitaka
litumie rasimu iliyotokana na maoni ya wananchi, alisema wanachama
watakaokuwa wakazi wa maeneo tofauti na wanayotaka kuyaongoza,
hawataruhusiwa.
Akihojiwa katika kipindi cha Maisha Mseto, Polepole alisema ili mwanaCCM
awe na sifa za kugombea, ni lazima awe mkazi wa eneo husika.
Polepole, ambaye alikuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba
iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba, alisema suala hilo lilikuwa sehemu
ya maoni ya wananchi wakati wa mchakato wa Katiba Mpya.
Alisema msisitizo mkubwa uliopo ni cheo kimoja kwa mtu mmoja jambo linalofundisha kuwa watu wenye kiasi.
“Haya mambo ndiyo watu wanayoyataka. Rais (John) Magufuli alienda mbele
zaidi kwamba utagombea nafasi ya uongozi kwenye eneo ambalo wewe ni
mkazi vinginevyo, marufuku kugombea,” alisema Polepole.
“Mwaka 2020 unakuja, si mtu upo zako Times FM unapiga kazi, halafu ikifika mwishoni unaenda Ileje eti unaenda kuchukua jimbo.”
Akizungumzia uamuzi huo, katibu wa wabunge wa CCM, Jason Rweikiza
alisema sharti hilo litakomesha tabia iliyojengeka kwa baadhi ya
wanachama wa chama hicho kwenda kugombea ubunge maeneo ambayo hawajui
yana matatizo gani.
“Unakuta wananchi wana shida ya maji, umeme na barabara anakuja mgombea
kipindi cha uchaguzi na ahadi kemkem, kumbe yote ni kuwavutia wampigie
kura na akishajihakikishia ushindi humumuoni tena,” alisema Rweikiza.
Rweikiza alisema hatua hiyo itasababisha watu wathamini kwao na kuelewa
matatizo ya maeneo waliyotoka na uchaguzi utakuwa huru bila ya rushwa.
0 comments: