Muhina ambaye ni mwongozaji watalii katika hoteli hiyo, alikuwa aondoke
na ndege ya Coastal Aviation saa nne asubuhi lakini viongozi wa hoteli
walimbadilishia ndege, hivyo aliondoka na Air Exel iliyofika salama
Serengeti.
Akizungumza na gazeti hili, meneja uendeshaji wa Hoteli ya andBeyond
Serengeti Under Canvas, Mussa Matala alisema Muhina ambaye anasomeka
kwenye orodha ya ndege kama Maina alikuwa apande ndege hiyo lakini
walimbadilishia.
Alisema waliomba aondolewe kwenye orodha ya wasafiri wa ndege hiyo
lakini kwa bahati mbaya hadi ndege ilipoondoka jina lake lilikuwapo.
Wakati huohuo, raia watano wa kigeni ambao walifariki dunia katika ajali
hiyo, akiwamo rubani Dewald Raubenheimer raia wa Afrika Kusini, ambaye
kwenye orodha ya awali ya waliofariki jina lake halikuwapo anatarajiwa
kusafirishwa leo.
Mhudumu wa chumba cha kuhifadhi maiti katika Hospitali ya mkoa ya Mount
Meru, Francis Costa alisema miili mitatu kati ya 11 imechukuliwa na
ndugu zao.
Alisema miili iliyochukuliwa ni ya ndugu wawili waliokuwa wakurugenzi wa Masai Wondering, Nasibu na Shatri Mfinanga.
Mwingine ni wa Joyce Mkama ambaye alikuwa mfanyakazi wa Hoteli ya Serena.
“Uchunguzi wa miili ya wageni kutoka nje ya nchi unaendelea na
ukikamilika itasafirishwa kwa mazishi katika nchi za Afrika Kusini,
Ujerumani na Italia,” alisema.
Ndege hiyo namba 5H-EGG aina ya Cessna Grand Caravan ilianguka baada ya
kugonga kingo za creta ya Empakai, umbali wa mita 3,250 kutoka usawa wa
bahari ikitoka Kilimanjaro kwenda Hifadhi ya Serengeti.
Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo alisema uchunguzi unaendelea kuhusu ajali hiyo.
Imeandikwa na Mussa Juma,Mwananchi
0 comments: