Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla Oktoba 22,2017 alitoa
kauli ya kufuta vibali vyote vya uwindaji kwa kampuni na kutoa siku 60
kwa watendaji ili waratibu mchakato upya utakaowezesha vitalu kugawiwa
kwa mnada.
Jana Jumatatu Novemba 6,2017 kupitia mitandao ya kijamii Dk Kigwangalla ametoa andiko linalosomeka ifuatavyo:
KWA UFUPI: Kuhusu Vitalu vya Uwindaji
Na Dkt. Hamisi Kigwangalla
Nimefuta
vibali vipya vya uwindaji vilivyokuwa vianze Januari 2018. Nitatangaza
upya mchakato mpya wa ugawaji vitalu kwa njia ya mnada - sasa hivi
wataalamu wetu wanatengeneza utaratibu utakaotumika kuuza vitalu kwa
njia ya mnada wa wazi. Pia, tunarekebisha sheria na kanuni kabla ya
kuanza mchakato mpya. Hivyo waliokuwa na vibali vya zamani, uhai wake
unaisha Disemba 31.
Kimsingi
mchakato wa vibali nilivyovifuta haukuwa halali kisheria, ulijaa rushwa
na upendeleo na haukuwa wa kimkakati, sababu Mpango wa Taifa wa miaka
mitano (2016 - 2021) unaelekeza twende kwenye njia ya mnada, BRN
inaelekeza twende kwenye njia ya mnada!
Wataalamu
walifaidika na utaratibu wa zamani - hawa walifanya tathmini ya nani
'ameendesha kitalu vizuri, nani ameendesha vibaya, hivyo wapendekeze kwa
waziri nani apate nani akose' (hapa kulikuwa na watu walitoa rushwa
mapema kabisa ili kujihakikishia wanapata vitalu; wanasiasa hususan
Mawaziri waliokalia hiki kiti zamani nao walifaidika na utaratibu huu wa
zamani (uliweka mazingira rahisi ya kuamua nani apate nani akose, na
maamuzi haya yalikuwa kwenye kichwa cha Waziri pekee - hapo mazingira ya
rushwa na upendeleo yalikuwa rahisi kabisa), wafanyabiashara na
wawekezaji kwenye sekta hii ya utalii wa uwindaji walikuwa wafaidika
wakubwa sababu walitupunja mapato ya ushuru (nchi zingine kitalu kidogo
tu kiliuzwa mpaka Dola 2,000,000, sisi tuliambulia Dola 60,000 tu.
Wanasiasa
na watu wajanja wanaojiita wazawa, ambao hata hawana weledi wala uwezo
wa kuwinda, walikuwa wakichukua vitalu (kwa ushawishi wao kwa Waziri)
kisha wanakikodisha kwa waendeshaji wa nje. Wengi walidai pango la hadi
Dola 300,000 kwa mwaka, huku wao wakilipa serikalini Dola 60,000 tu.
Utaratibu
huu wa zamani uko kinyume kabisa na tafiti mbalimbali zilizofanyika
miaka ya mwishoni mwa tisini na mwanzoni mwa miaka ya 2000. Leo zaidi ya
miaka 20 hakuna aliyethubutu kubadilisha utaratibu. Sababu kubwa ni
syndicate ya wanufaika, tena wachache wale wale tu. Ikawa maeneo haya
wamejimilikisha kama yao milele.
Uamuzi
wangu kuufuta utaratibu huu ni dhahiri umewaudhi wengi na najua
watanishambulia sana. Naombeni dua zenu. Tanzania ilihitaji mmoja wetu
afike mahali aseme 'sasa basi' na tutake tusitake iwe hivyo, Rais
Magufuli amejitoa, Mimi namuunga mkono kwa 'vitendo', nasema sasa basi!
Nitamsaidia kazi hii kwa uaminifu, uadilifu, uzalendo na weledi wa hali
ya juu. Si amenipa kazi, kazi nitafanya! Dua zenu tu.
0 comments: