Dodoma, Novemba 14, 2017:
Serikali imesema mapato yatokanayo na kodi ya majengo yanayokusanywa na
Serikali yameongezeka baada ya jukumu hilo kukabidhiwa kwa Mamlaka ya
Mapato Tanzania (TRA), ikilinganishwa na ilivyokuwa chini ya
Halmashauri.
Hayo
yameelezwa Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango,
Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji (Mb), alipokuwa akijibu swali la msingi la
Mbunge wa Bukoba Mhe. Wilfred Lwakatare (CHADEMA), aliyetaka kujua
Serikali inazipa Halmashauri ushauri gani wa kitaalam wa hatua za
kuchukua ili kuziba pengo la kibajeti.
Katika
swali hilo Mhe. Lwakatare aliuliza kuwa Serikali haioni kuwa uamuzi wa
kuipa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kukusanya kodi hiyo ya majengo
ni kuzidi kuipa mzigo mkubwa ambao hawatauweza.
Dkt.
Kijaji alisema kuwa baada ya makusanyo yatokanayo na kodi za majengo
kuanza kukusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA katika Halmashauri
za Miji, Manispaa na Majiji 30, yalipanda hadi kufikia Sh. bilioni 34.09
mwaka wa fedha 2016/2017 ikilinganishwa na Sh. bilioni 28.28
zilizokuwa zimekusanywa na Serikali za Mitaa mwaka wa fedha 2015/2016.
“Makusanyo
hayo ni sawa na ongezeko la asilimia 20.6 ya makusanyo halisi
yaliyopatikana kutoka Halmashauri husika kabla ya kodi hiyo kuhamishiwa
TRA hali inayodhihirisha kuwa, TRA imefanya kazi nzuri katika kukusanya
mapato ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa na Halmashauri hizo 30
katika mwaka wa fedha 2015/16.”. alisema Dkt. Kijaji.
“Katika
robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2017/18 Julai hadi Septemba, TRA,
ilipangiwa kukusanya kodi ya majengo ya kiasi cha Sh. Bil 11.9 na
kufanikiwa kukusanya kiasi cha Sh. Bil. 13.2 ikiwa ni ufanisi wa
asilimia 111”. Aliongeza Dkt. Kijaji.
“Hatua
ya Serikali ya kukasimu jukumu la ukusanyaji wa kodi za majengo kwa
TRA, haikulenga kuzinyang’anya Halmashauri vyanzo vya mapato bali ni
kuimarisha ukusanyaji wake”. alisema Dkt. Kijaji.
Aliongeza
kuwa dhamira ya Serikali ni kuhakikisha kunakuwepo ufanisi katika
ukusanyaji na matumizi ya kodi zote zinazokusanywa ndani ya Serikali na
kwamba Halmashauri zote zinapata mgao wa fedha kwa kuzingatia makisio ya
bajeti zao na makusanyo ya mapato yote ya Serikali.
Aidha,
Dkt. Kijaji alisema kuwa Serikali inatambua kuwa kodi ya majengo
imekuwa ikichangia kwa sehemu kubwa mapato ya Halmashauri za Miji,
Manispaa na Majiji katika kutekeleza mipango na utoaji wa huduma na
maendeleo kwa wananchi.
Katika
swali la nyongeza Mhe. Lwakatare alihoji kwa nini Serikali isichukue
maoni yake ya baadhi ya majengo makubwa yatozwe kodi na TRA na yale
madogo yatozwe kodi na Halmashauri kwa kuwa kumekuwa na changamoto kwa
TRA katika ukusanyaji wa kodi hiyo na kuwatumia Maafisa Watendaji wa
Kata katika kukusanya kodi hizo ambao wameajiriwa na Halmashauri.
Akijibu
swali la nyongeza Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali na Bunge
lilipitisha sheria ya fedha kwamba kodi ya majengo ikusanywe na TRA kwa
lengo la kuimarisha ufanisi wake katika ukusanyaji na matumizi.
“Serikali
itaendelea kusimamia sheria hiyo na kuhakikisha lengo la kuchukua kodi
hiyo linafanikiwa na wananchi wanapata huduma stahiki”. aliongeza Dkt.
Kijaji.
Imetolewa na:
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
0 comments: