Mfanyakazi
wa kampuni ya saruji ya Simba Cement, Edward Ngassa amekamatwa na Jeshi
la Polisi mkoani Dodoma kwa tuhuma za kutengeneza tukio la uongo la
kuporwa Sh. milioni 20.4 na majambazi jana.
Kwa
mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto, mbwa wa
polisi mwenye mafunzo ndiye aliyegundua udanganyifu huo wa Ngassa
nyumbani kwake.
Kamanda
Muroto alisema mtuhumiwa huyo alitengeneza tukio la uongo kwamba
ameporwa fedha na majambazi katika eneo la Uhindini karibu na mgahawa wa
Sunja.
Kufuatia
ripoti ya tukio hilo, Muroto alisema, timu ya upelelezi ilifanya
uchunguzi wa kina na kubaini kwamba hakukuwa na tukio la uporaji katika
eneo hilo.
“Katika
uchunguzi huo tulienda kumpekua kwa kina mtuhumiwa nyumbani kwake na
kufanikiwa kukamata fedha zote alizoiba akiwa ameficha kwenye ndoo ndogo
ya plastiki na kuweka udongo kisha kupanda ua juu yake ili zisikamatwe
kirahisi,” alisema.
Muroto
alibainisha kuwa waliweza kuzifichua fedha hizo kwa kutumia mbwa ambaye
alikuwa akinusa kwenye maeneo yote na kuzikuta kwenye ndoo ya ua.
“Huyu
mtuhumiwa alimpigia simu mwajiri wake akidai kuwa wakati anaelekea
benki kuna pikipiki ya majambazi ilimzuia kwa mbele na kumpora hizo
fedha,” alisema Muroto.
Katika
hatua nyingine, Kamanda Muroto alisema watu wawili wamekamatwa kwa wizi
wa betri tatu za minara ya mawasiliano katika eneo la Chang’ombe na
Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom).
“Watuhumiwa
Eliezel Muhongole ambaye ni fundi na mfanyakazi wa kampuni ya Halotel
na Alfredy Mlugu mkulima na mkazi wa Mpunguzi walikamatwa kwa wizi huu,”
alisema Muroto.
Mbali
na hilo, Muroto alisema watu watatu wanashikiliwa na polisi mkoani humu
kwa kukamatwa na vipande vinne vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo
16 na thamani ya Sh. milioni 33.2.
Aliwataja
waliokamatwa kuwa ni mkazi wa Dar es salaam Hussein Henry (40), na
Mussa Ramadhani (35) na Abdalah Ramadhani (32) wote wakazi wa Kondoa.
“Hawa
walikamatwa wakiwa wamepakia meno haya ya tembo kwenye pikipiki yenye
namba za usajili MC516 BDC aina Fekon wakitokea Kondoa wakielekea Dodoma
mjini,” alisema.
0 comments: