ATHUMAN BEMELENGO - DAUDA.COM
0713 094952
0713 094952
Majuma kadhaa yaliyopita nilipata kuwatazama wachezaji
wawili bora zaidi kwasasa ulimwenguni. Lionel Messi na Cristiano
Ronaldo. Nilimuona Messi aliyecheza dhidi ya Juventus ambaye kimsingi
hakucheza kwa kiwango bora. Pia nilimuona Ronaldo aliyecheza dhidi ya
Bayern Munich.
Unaweza kusema walikuwa binadamu tofauti sana na wale
tuliozoea kuwaona kila mmoja kwa michezo waliyocheza. Lakini ndio
uhalisia. Messi dhidi ya Juventus alikuwa mchezaji wa kawaida sana
ambaye usingeweza kuamini kama ndio yeye kama ndio ingekuwa mara ya
kwanza kumuona baada ya kusimuliwa maajabu yake.
Cristiano Ronaldo yeye alikuwa na usiku mzuri dhidi ya
Bayern Munich baada ya kuiwezesha timu yake kufuzu hatua ya nusu fainali
dhidi ya timu bora kama Bayern Munich tena akiwa amefunga magoli matano
katika michezo yote miwili. Sio kitu rahisi kufunga magoli matano mbele
ya kipa mwenye kiwango cha Manuel Neuer.
Ulikuwa usiku pekee ambao ungeweza kumpata mshindi katika
ile debate ya ubora wa hawa wafalme wawili. Mtizame Ronaldo, licha ya
kuwa na umri mkubwa lakini anaonekana bado ana uwezo mkubwa wa kucheza
na kufunga tofauti na Messi ambaye anaonekana kabisa kasi yake
imepungua.
Kabla ya El Classico ungeweza kuamini Messi hana jipya tena
zaidi ya ndevu zake kuwa maajabu pekee aliyobakiza. Huu ndio ulikuwa
wimbo wa wale waliomdhihaki.
Niliulizwa sana, Ni kweli Messi alikuwa ameisha? Jibu
sahihi lilikuwa hapana, Nikaulizwa tena, sasa tatizo ni nini? Na kwa
nini Ronaldo licha ya kuwa na umri mkubwa zaidi anaonekana kuwa bora?
Hayo ni baadhi ya maswali niliyoulizwa na waliotaka kujua
kwa nini nilikuwa nikisema Messi bado hajaisha na anaweza kuendelea kuwa
mshindani sahihi wa Ronaldo wakiitafuta pensheni yao.
Suala ni moja tu, Ronaldo kwa upande wake yeye amejua namna
sahihi ya kucheza kwa wakati huu ambao umri umeanza kumtupa mkono.
Ronaldo wa sasa hivi hakimbii sana wala hakai sana na mpira. Unaweza
usimuone timu ikicheza mpira na ukalazimika kumuona akifunga tu.
Analazimika kugusa mpira mara chache sana hasa pale
inapobidi. Real Madrid tayari inao watu wanaoweza kumfanya Ronaldo
asilazimike kuuchezea zaidi mpira na akasubiri tu mbele ya goli la timu
pinzani ili afunge.
Miguu ya Toni Kroos na Luka Modric inafanya kazi kubwa kuhakikisha
inautawanya mpira katika maeneo yote ya uwanja huku Marcelo na Carvajal
wakiwa na jukumu la kupeleka mipira salama kwa Ronaldo.
Hivi ndivyo Real Madrid ilivyojiandaa kumfaidi zaidi
Ronaldo akiwa anaelekea katika uzee wake. Unafikiri hawakuujua umri wake
walipoamua kumpa mkataba mrefu mpaka mwaka 2022? Hawezi kuwa Florentino
Perez anayeweza kufanya biashara ya kiuendawazimu.
Wanaweza kuwatumia Isco na James Rodriguez ili Ronaldo
apate muda wa kupumzika. Hii ndio njia sahihi ya kuwatumia wachezaji
walioanza kuishi mbali na zama zao. Hawahitaji kukimbia sana uwanjani,
kufanya kazi nyingi uwanjani au kucheza muda mrefu bila kupumzika.
Madrid tayari wanalijua hili na wameshaona wamefanikiwa na
ndio maana wanapata jeuri ya kuamini hawana haja ya kutumia nguvu nyingi
kuzipata nyayo za Eden Hazard kuliko mikono salama ya David De Gea.
Ukimuangalia Messi unaweza kudhani ni mkubwa kuliko Roaldo
lakini shida yake ameanza kutumika mapema sana. Akiwa na miaka 19
alishaingia katika rekodi ya kufunga hat trick kwenye El
Classico.Barcelona wamejisahau sana.
Waliamini kile kizazi alichokitengeneza Pep Guardiola akiwa
kocha wa vijana pale Catalunya kingeishi milele. Hakuna kizazi
kilichoandaliwa kuja kurithi zama zao.Messi anahitaji kupumzika, kuugusa
mpira mara chache katika maeneo hatari zaidi na akiwa hakimbizani tena
na mabeki.
Lakini mambo ni tofauti sana. Barcelona ya sasa inamhitaji
zaidi Messi kuliko unavyofikiri. Matokeo yake wamemfanya kuwa mtumwa,
anateseka sana. Wanamhitaji afunge, aichezeshe timu na ikibidi akabe
pia. Unampata wapi tena Messi anayeweza kufanya yote haya wakati hata
yule wa ubora wake hakuweza.
Barcelona haina tena mashine zake zilizoifanya kuwa tishio
kuanzia kwenye eneo la kiungo. Sergio Bosquets na Andres Iniesta tayari
wamejichokea. Huwezi tena kuziona miguuni mwao zile pasi zilizomtia
‘Degedege’ Sir Alex Ferguson pale Wembley mwaka 2011. Ni vijana wa kiume
pekee walioweza kumtetemesha mwanaume Sir Alex Ferguson.
Ni nani anaweza kuifanya ile kazi aliyokuwa akiifanya pass
master Xavi Hernandez ambaye alikuwa na uwezo wa kukimbia uwanja mzima
akiwa amepiga pasi nyingi zaidi ya timu pinzani?
Sio Ivan Rakitic wala Andre Gomes anayeweza hata kujaribu
ila inabaki kuwa kazi nyingine ya Lionel Messi. Unaikumbuka mechi dhidi
ya PSG? Luis Enrique alimuanzisha Messi katika eneo la kiungo kuifanya
kazi hii huku Rafinha akianzishwa katika safu ya ushambuliaji sambamba
na Neymar na Luis Suarez.
Siku ile Messi alikuwa mtu muhimu zaidi uwanjani huku
Neymar akiwa mchezaji bora. Sio Iniesta wala Rakitic ambaye angeweza
kuwashinda Verrati na Rabiott pale kati ya dimba.Ulimuona Messi dhidi ya
Real madrid?
Kupitia kwake utakiona nilichokueleza hapo juu. Alihitajika
kumsaidia Iniesta katika eneo la kiungo ili kuiunganisha timu kutoka
eneo la kiungo hadi mbele. Ilikuwa kazi rahisi sana kwa uwezo wake.
Alimaliza mechi akiwa ametimiza magoli 500 ya La liga na magoli 23
aliyofunga kwenye El Classico.
Messi bado ana uwezo wa kuendelea kucheza kwa muda mrefu
tena kwa kiwango kikubwa hata zaidi ya Cristiano Ronaldo kama Barcelona
watatafuta namna sahihi ya kumtumia kwa kipindi hiki ambacho anaonekana
umri umeanza kuachana na kasi yake.
Njia pekee na sahihi ni kuijenga timu upya itakayomhitaji
Messi kutumia zaidi akili yake na ubunifu kufunga magoli bila kutumia
nguvu kubwa. Kama wataona hawahitaji kufanya hivyo kutokana na uwepo wa
Neymar, basi watakuwa wanajiongopea.
Nani ataweza kuutawanya mpira katika maeneo yote ya uwanja
kama walivyokuwa wakifanya Xavi na Iniesta? Neymar pekee? Hatoweza
kuifanya hata anayoifanya Messi sasa hivi.
Wanahitaji damu changa kama Thiago Alcantara na Marco Verrati au Hector Bellerin bila kusahau watu imara katika safu ya ulinzi.
Ukiwa na watu wa aina hii, ni lini Messi atalazimika
kushuka kwenye eneo la kiungo kukimbizana? Hii ndio njia sahihi
itawafanya Barcelona waendelee kumfaidi Messi kwa muda mrefu zaidi.
0 comments: