WAANDISHI WATAKIWA KUTUMIA KALAMU ZAO VIZURI
Na Nuru Juma & Husna Saidi- MAELEZO
Waandishi wa Habari nchini wametakiwa
kuzingatia kanuni,sheria na taratibu za uandishi katika kuandika habari
zitakazoleta umoja,mshikamano na maendeleo na siyo uchochezi ili kujenga
jamii bora.
Hayo yamesemwa leo Jijini Mwanza na
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt.Harrison George
Mwakyembe kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya
Habari Duniani.
Dkt. Mwakyembe aliongeza kwa kusema kuwa
Serikali inatambua umuhimu wa siku ya uhuru wa vyombo vya habari ambapo
siku hiyo huwa maalum kwa wadau wa tasnia hiyo kukutana na kujadiliana
mambo mbalimbali ikiwa ni njia ya kujenga jukwaa la ushirikiano.
“Uhuru wa habari una ukomo wake hivyo ni
muhimu kwa vyombo vya habari hapa nchini kuajiri watu wenye taaluma
hiyo kwa kuachana na makanjanja ili viheshimike kwa kutoa taarifa zenye
kuzingatia maadili ya uandishi”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Alizidi kufafanua kuwa katika
kuadhimisha siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, kalamu ya
mwandishi wa habari itetee ukweli na si mambo ya haramu kwa sababu ya
siasa au rushwa ambayo huwa kichocheo cha uvunjifu wa amani.
Aidha aliitaka Idara ya Habari (MAELEZO)
kuwa na utaratibu wa kukutana na wahariri kila mwezi ili kuweza
kujadili changamoto mbalimbali zinazoikabili tasnia nzima ya habari
nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya
Habari (MAELEZO) Dkt. Hassan Abbasi alisema uandishi wa habari si
biashara ya kawaida bali ni kazi yenye kuhitaji uweledi mkubwa hivyo
waandishi wanatakiwa kufuata taratibu na sheria za uandishi.
0 comments: