Mwenyekiti wa CHADEMA Mhe. Freeman Mbowe amefunguka na kusema kuwa ile hofu iliyokuwepo Mbunge Tundu Lissu aliyeshambuliwa na risasi kuwa huenda angepoteza maisha imezidi kupungua na kudai madaktari wanatoa matumaini makubwa hali yake inaimarika.
Freeman
Mbowe amesema hayo leo kupitia kwenye mitandao yake ya kijamii na
kusema kuwa Mbunge huyo sasa anaweza kuzungumza japo anaendelea kupatiwa
matibabu na kudai pia ataendelea kufanyiwa upasuaji mwingine, aidha
Mbowe amewataka wananchi kutosikiliza taarifa za watu wengine kuhusu
hali ya mgonjwa na kusema taarifa rasmi juu ya hali ya mgonjwa itatolewa
na wao ambao wapo na mgonjwa Nairobi Kenya.
"Kuhusu
hali ya Mhe. Lissu, kwa sasa ile hofu ya kupoteza maisha imezidi
kupungua, madaktari sasa wanatoa matumaini makubwa kuwa hali yake sasa
inaimarika. Yale yote yaliyokuwa yanatishia pengine uhai wake, usalama
wake, yamepungua kwa kiasi kikubwa na madaktari wanatoa matumaini
makubwa. sasa hivi, Mhe Lissu anaweza kuzungumza, nimezungumza nae, japo
bado anapatiwa matibabu na ataendelea kwenda 'theatre' kwa ajili ya
upasuaji na kutibu majeraha mbalimbali aliyoyapata. Anazungumza na
anatoa salamu kwa Wanaafrika Mashariki, anatoa salamu kwa Watanzania,
niseme tu kwamba sisi ambao tuko nae muda wote ndo tunajua hali halisi
ya mgonjwa" alisema Freeman Mbowe
Mbali
na hilo Freeman Mbowe amedai kuwa Mbunge huyo hana athari zozote zile
kwenye kifua chake kama ambavyo baadhi ya taarifa zinasema kwenye
mitandao mbalimbali ya kijamii na kudai Mwanasheria Mkuu huyo wa CHADEMA
yupo imara.
"Mhe.
Lissu hana 'infection' ya kifua, kwa sasa yuko vizuri yuko imara, bado
ni 'critical' lakini bado yuko stable. Tuendelee kumuombea kila siku,
wakati wote, aweze kupona kwa haraka na kuruhusiwa kutoka hospitali" alisema Mbowe
Mbunge
Tundu Lissu alishambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7,
2017 akiwa Makao Makuu ya nchi mjini Dodoma na baadaye kusafirishwa
kwenda jijini Nairobi Kenya kwa ajili ya kupatiwa matibabu kufuatia
majeraha aliyopata, ambapo mpaka sasa yuko huko kwa matibabu.
0 comments: