WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy
Mwalimu amesema serikali ipo tayari kuhudumia kwa kiasi chochote cha
fedha matibabu ya kibingwa kwa ajili ya Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu (Chadema), endapo itapokea ombi rasmi kuanzia sasa.
Amesema kimsingi serikali haijapokea ombi lolote rasmi kutoka kwa
familia lililoambatana na taarifa ya madaktari kuthibitisha kiongozi
huyo anahitaji huduma za matibabu ya kibingwa zaidi katika nchi yoyote
duniani, licha ya kwamba imekuwa tayari kufanya hivyo mara moja tangu
lilipotokea tukio la kujeruhiwa kwa risasi mbunge huyo.
Alitoa kauli hiyo alipozungumza katika mkutano na waandishi wa habari
jijini Tanga uliolenga kutoa ufafanuzi kwa Watanzania pamoja na familia
ya Lissu kuhusu msimamo wa serikali katika matibabu ya kiongozi huyo.
Ummy ambaye yuko jijini Tanga kwa shughuli za kikazi za uchaguzi wa
jumuiya za Chama Cha Mapinduzi (CCM), alisema wizara yake imeona ni vema
kuzungumzia suala hilo kutokana na kuibuka kwa taarifa mbalimbali
zinazolenga kupotosha jamii na ulimwengu kuhusu matibabu ya Lissu
yanaoendela katika hospital iliyoko Nairobi nchini Kenya.
“Naomba nichukue nafasi hii kuwajulisha Watanzania kwamba serikali
haijakataa wala haijashindwa kugharamia matibabu ya Mheshimiwa Lissu
kama inavyodaiwa na baadhi ya watu hivi sasa, taarifa tunazopata mpaka
sasa kiongozi hiyo anaendelea na matibabu yake huko Nairobi, lakini
kidogo tunaona kunafanyika mambo yasiyoeleweka ikiwemo hasa dhamira ya
kufanywa kwa mambo hayo, hivyo naomba kupitia mkutano huu mfikishe
ujumbe kwamba serikali iko tayari kumhudumia popote duniani anapotaka
kupelekwa kupata matibabu ya kibingwa endapo tu tutapata maombi rasmi
kutoka kwa familia yake,” alieleza waziri huyo.
Alisema upo utaratibu maalumu ambao serikali inawajibika kuufuata ili
kumsaidia Mtanzania yeyote anayehitaji matibabu ya kibingwa nje ya nchi,
lakini tofauti iliyojitokeza kwenye suala la Lissu baada ya kulazwa
katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, ndugu na jamaa zake ndiyo
waliomchukua kumpeleka Kenya.
“Pamoja na nia ya serikali ya kutaka kumpeleka Lissu katika Hospitali ya
Taifa ya Rufaa Muhimbili, ndugu na jamaa wa karibu walifanya
majadiliano na kuamua badala ya kupelekwa huko na serikali wao walipenda
kumpeleka Nairobi... hivyo kama serikali hatukuwa na uamuzi wowote au
nguvu zaidi ya kumzuia mgonjwa huyo asipelekwe katika hospitali ya
Nairobi hivyo mgonjwa aliruhusiwa kuondoka usiku huo huo majira ya saa
tano na nusu usiku kwa ndege,” alieleza.
Aliongeza kuwa pamoja na mambo yote hayo, si vema suala la matibabu ya
Lissu likaendelea kuchukuliwa kisiasa hasa kwa kuendelea kusambaza
taarifa za upotoshaji kwa jamii wakati utaratibu wa serikali upo wazi na
unafahamika.
Akizungumzia michango mbalimbali ya fedha inayoendelea kuhamasishwa na
watu mbalimbali nchini, waziri ameiomba familia hususan mke wa Lissu
kuwasiliana moja kwa moja na serikali ili kueleza mahitaji ya mahali
popote duniani wanapotaka kumpeleka mgonjwa wao ili kuokoa maisha yake.
“Serikali inahudumia matibabu yake pale inapohitajika kwa sababu licha
ya kuwa ni Mtanzania, lakini ieleweke kwamba Lissu ni mbunge, lakini cha
kushangaza tumeona inapitishwa michango kadha wa kadha inayolenga
kukusanya fedha za matibabu hatuelewi michango hiyo inaweza kutumika
vibaya, kiutapeli wakati serikali hatujashindwa kutekeleza jukumu hili,”
alifafanua waziri mwenye dhamana ya Afya.
“Nimuombe mke wa Lissu, dada Alice najua uko katika wakati mgumu sana,
lakini naamini utaifikia serikali ili kuhakikisha kwamba tunamsaidia
Lissu apate matibabu katika nchi yoyote duniani iwe India, Ujerumani au
popote duniani serikali itagharamia,” aliongeza.
Spika Job Ndugai alitangaza bungeni kwamba wabunge wote wana bima ya
afya na kwamba wanatibiwa katika hosptali ya Taifa ya Muhimbili na kama
kuna ulazima wa kupelekwa nje ya nchi, wabunge wote hutubiwa katika
hosptali ya Apollo ya India.
Alisema familia ya Lissu ndiyo iliyoomba kumpeleka Nairobi. Naye
Mwandishi Wetu, Katuma Masamba anaripoti kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania,
Profesa Ibrahim Juma amesema Mahakama haiwezi kutoa maoni kwa jambo
ambalo liko kwenye utaratibu wa kufikishwa mahakamani, kwa kuwa kanuni
za mahakama haziruhusu jambo hilo.
Jaji Juma alitoa kauli hiyo wakati akijibu swali kuhusu ukimya wa
mahakama juu ya tukio tukio la Lissu ambaye ni Rais wa Chama cha
Wanasheria Tanganyika (TLS) kupigwa risasi na barua ya Chama cha
Wanasheria wa Marekani ya kulaani tukio hilo, huku akitaka jamii kutulia
na kuachia mamlaka husika kufanya kazi yake.
Akijibu maswali ya wanahabari jana Dar es Salaam, Jaji Juma alisema
kanuni za mahakama haziruhusu jambo ambalo litakuja mahakamani kutolewa
ushahidi, kuongelewa au kutolewa maoni kwa kuwa ni kinyume cha kanuni.
Kuhusu uhuru wa mahakama, alisema mahakama ziko huru na hakuna jaji
yeyote anayeweza kumuingilia hakimu yeyote na kumueleza namna ya kufanya
na kwamba mhimili huo unafanya kazi zake kwa uwazi kuliko mihimili
mingine. Katika hatua nyingine, Mkutano wa Chama cha Majaji na Mahakimu
wa Jumuia ya Madola (CMJA) utafanyika Dar es Salaam kuanzia Jumatatu.
IMEANDIKWA NA ANNA MAKANGE - HABARILEO TANGA
0 comments: