WAZIRI MKUU ATAKA ULINZI KUIMARISHWA KWENYE VIWANDA
WAZIRI mkuu,Kassim Majaliwa amezitaka serikali za vijiji na ngazi nyingine mkoani Pwani,kujikita kuimarisha ulinzi katika maeneo mbalimbali ikiwemo ya viwanda ili kulinda mali na usalama wa wawekezaji na watanzania kijumla.
Amesema haijajulikana hadi sasa nia na dhamira ya watu wasiojulikana wanaojihusisha kupoteza maisha ya watu ,na ni hatari endapo watajiingiza katika maeneo ya uwekezaji kwani hakuna mwenye uhakika wa azma yao.
Aidha Majaliwa ,ametoa wiki mbili kwa waziri wa maji kutathmini matokeo ya mwenendo wa mradi wa maji wa WAMI ,ili kutoa utaratibu na kama sheria inaruhusu kuvunja mkataba ikiwa mkandarasi ameshafikia kiwango cha asimilia 50 ya utekelezaji.
Waziri huyo ,pia ameziagiza halmashauri nchini kuona umuhimu wa kutenga fedha kwa ajili ya kununua magari ya zimamoto yatakayosaidia kudhibiti majanga ya moto yanapotokea hususan kwenye maeneo ya uzalishaji na viwanda.
Katika hatua nyingine amelitaka shirika la umeme Tanesco,Dawasco kuhakikisha wanaboresha miundombinu ya umeme na maji katika maeneo yenye uwekezaji ili kuvutia wawekezaji.
Alitoa rai hiyo,wakati wa ziara yake ya siku moja ,aliyoifanya mkoani Pwani kutembelea kiwanda cha kutengeneza sabuni cha KEDS kilichopo Kibaha,na cha kutengeneza vigae Twyford Ceramics Ltd/Pingo,Chalinze ,Bagamoyo.
Majaliwa ,alieleza kuwa ni lazima raia mmoja mmoja na jukumu la kila mmoja kusimamia kulinda nchi kuanzia maeneo wanayoishi .
Alisema serikali imejipanga kuendelea kusimamia amani na utulivu,ambapo amewataka wananchi waiunge mkono serikali kupambana na wahalifu wasio na nia njema na serikali.
“Hatuna uhakika kwa watu hawa wanaofanya vitendo vya ovyo,watanzan ia waungane na serikali,kupambana ili wasije kuingia kwa wawekezaji na kupoteza ndoto za serikali za kupata wawekezaji “alisema Majaliwa.
Akizungumzia tatizo la uhaba wa maji ,alisema mradi wa WAMI ulikuwa ukamilike tangu mwezi July mwaka huu.
Alisema alitembelea mradi huo mwezi juni mwaka huu ukiwa chini ya asilimia 38 na kusema mkandarasi akiendelea kusuasua watamfukuza na kutoa agizo ikifika mwezi huu wafikie asimilia 80.
“Nilitaka kuja mwezi huu lakini nikaambiwa speed ni ndogo na bado hali hairidhishi,na mkandarasi hajamaliza”mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete amekuwa akiuliza juu ya kukwama kwa mradi huo” ;”Nimetoa wiki mbili kwa waziri aangalie dhamana ya kampuni kwenye ubalozi wao wa India na kuangalia sheria namna ya kufanya ama kukamilisha mradi kwa muda mfupi uliobaki”alifafanua.
Kuhusu nishati ya umeme Majaliwa,alisema serikali ipo mbioni kutekeleza mradi mkubwa wa umeme stiegler’s gorge katika chanzo cha mto Rufiji, utakaozalisha megawatts 2,100 zitakazoondoa kama si kumaliza upungufu wa umeme uliopo.
Aliitaka halmashauri ya Chalinze,ijipange kwa matumizi bora ya ardhi ili kuondoa migogoro na kuondoa usumbufu kwa wawekezaji.
Kuhusu suala la zimamoto ,Majaliwa alisema mkoa huo kwasasa una viwanda vikubwa hivyo wakati serikali ikipokea changamoto ya uhaba wa vifaa na magari ya zimamoto ,halmashauri ijipange kupitia bajeti zao.
“Viwanda hivi ni vikubwa vinajengwa ,kiwanda hiki cha KEDS kina jengo hilo hapo lenye urefu wa mita 30 juu,tuombe mungu moto usitokee ,unawezaje kuzima moto kwa maji ya kwenye ndoo ,ipo haja ya kuangalia namna ya kutatua changamoto hii”
“Dar es salaam ambako ni mji wa kibiashara serikali itasaidia katika kununua mitambo ya kusaidia kuzima moto kutegemea ukubwa wa majengo yaliyopo”aliongeza Majaliwa.
Kwa upande wa miundombinu ya barabara,alitoa rai kwa halmashauri ya Mji wa Kibaha kuboresha barabara zilizopita mitaani na kuhakikisha mitaa yote iwe na barabara bora kwa kufumua zisizofaa na kuchonga barabara zenye viwango.
Pamoja na hayo ,Majaliwa alibainisha uwekezaji kama huu unaendana na dhana ya Rais Dk John Magufuli wa kuifanya nchi kuwa ya Viwanda ambapo itaongeza pato la nchi na itazalisha ajira kwa wingi.
0 comments: