NIMEAMUA
kujiuzulu NAFASI yangu ya Ujumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha
Mapinduzi CCM, pamoja na nafasi zote za Uongozi ndani ya Chama kuanzia
leo, Oktoba 30, 2017.
HALIKADHALIKA,
asubuhi ya leo nimemwandikia Spika wa Bunge, Mh. Job Ndugai, Mb., barua
ya kujiuzulu nafasi yangu ya UBUNGE wa Jimbo la Singida Kaskazini
kupitia tiketi ya CCM, nafasi ambayo nimeitumikia kwa vipindi vinne
mfululizo tangu nilipochaguliwa kwa mara ya kwanza mnamo mwaka 2000 hadi
Sasa.
AIDHA,
Nimechukua UAMZI huo kutokana na kutoridhishwa kwangu na mwenendo wa
hali ya Kisiasa nchini, ikiwa ni pamoja na ukiukwaji wa HAKI za
Kibinadamu, ongezeko la vitendo vya dhuluma wanavyofanyiwa baadhi ya
watanzania wenzetu, na kutokuwepo kwa mipaka ya wazi kati ya MIHIMILI ya
dola (Serikali, Bunge, na Mahakama) kunakofanya utendaji kazi wa
Kibunge wa Kutunga Sheria na wa Kuisimamia Serikali kutokuwa na uhuru
uliainishwa na kuwekwa bayana KIKATIBA.
VILEVILE,
Naamini kwamba bila Tanzania kupata Katiba Mpya Sasa, hakuna namna
yeyote ya kuifanya mihimili ya dola isiingiliane na kuwepo kwa ukomo wa
wazi na kujitegemea kwa dhahiri kwa mihimili ya Serikali, Bunge na
mahakama ambayo ndio chimbuko la Uongozi Bora wa nchi, na kuonesha kwa
uwazi kuwa madaraka yote yatokana na wananchi wenyewe, na kwamba
Serikali ni ya Watu kwajili ya Watu.
MIMI
Naondoka na kukiacha Chama Cha Mapinduzi CCM, nikiwa nimekitumikia
kuanzia ngazi ya Uenyekiti wa UVCCM Mkoa, Ujumbe wa Kamati za Siasa
Wilaya na Mkoa, Ujumbe wa Kamati ya Wabunge Wote wa CCM na Mjumbe wa
Halmashauri Kuu ya CCM TAIFA, kwani nimejiridhisha kuwa kwa mwenendo wa
hali ya kisiasa, kiuongozi na kiuchumi uliyopo Tanzania Sasa, CCM
imepoteza mwelekeo wake wa kuisimamia Serikali kama ilivyokuwa hapo
awali.
AIDHA,
Naamini kuwa, kama ilivyotokea kwa mihimili ya Bunge na Mahakama
kutokuwa na uhuru kamili, bila kuingiliwa kiutendaji kwa namna Moja au
nyigine, CCM nayo imekuwa Chini ya miguu ya dola badala ya chama kushika
hatamu na kuikosoa Serikali inapobidi kama yalivyokuwa maono ya Baba wa
TAIFA MWALIMU Julius Kambarage Nyerere.
HIVYOBASI,
kwa dhamira yangu, na kwa uamuzi wangu mwenyewe, nikiwa na haki ya
KIKATIBA, natangaza KUKIHAMA Chama Cha Mapinduzi CCM leo hii, na
nitaomba IKIWAPENDEZA wanachama wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo
CHADEMA, basi waniruhusu kuingia MALANGONI mwao, niwe mwanachama, ili
kuungana na CHADEMA na watanzania wote wanaopenda kuleta mabadiliko ya
kisiasa na kiuchumi nchini kwa kupitia mfumo wa ki demokrasia na uhuru
wa mawazo.
VILEVILE,
nimemua kujiuzulu KITI Cha Ubunge, Jimbo la Singida Kaskazini kuruhusu
kufanyika kwa UCHAGUZI mwingine ili wananchi wapate fursa ya kuchagua
ITIKADI wanayoona inawafaa kwa majira na nyakati hizi zenye changamoto
lukuki nchini Tanzania. Ni imani yangu, kamwe hayatakuwa ya bure maneno
haya, wala uamuzi huu niufanyao mbele ya Watanzania leo ili kwamba, SOTE
kama TAIFA tuingie kwenye mjadala wa kuijenga upya misingi ya nchi
yetu.
0 comments: