
Kesi ya kuua bila kukusudia inayomkabili muigizaji wa filamu Tanzania,
Elizabeth Michael (Lulu), imeendelea jana ambapo upande wa mshtakiwa
umeanza kutoa utetezi wake.
Akisimulia jinsi ilivyokuwa siku ya tukio, Lulu amesema marehemu alikuwa
akimpiga na panga baada ya kutokea ugomvi uliotokana na wivu wa
mapenzi, alipomuona akiongea na simu.
"Nilikuwa nataka kutoka ila marehemu 'Kanumba' alinikataza, alikuwa
hataki nitoke, nilipomwambia natoka na marafiki zangu alinikimbiza na
taulo na mimi nilikuwa naogopa kupigwa, mara nyingi alikuwa ananipiga
kila akilewa na sio kwa akili zake, alipoona simu yangu inaita akahisi
ni simu ya mwanaume akasema kwanini naongea na simu ya mwanaume mbele
yake? Marehemu akaingia uvunguni akatoa panga akasema leo nakuua huku
akinipiga na panga kwenye mapaja", ameelezea Lulu.
Lulu ameendelea kusimulia...."Marehemu alianguka mwenyewe na kujigonga
kwa nguvu na kuinuka sehemu nyingine alikuwa kama anatapatapa,
nilimwambia Seth kuwa Kanumba amedondoka na akajaribu kumuamsha hakuamka
akasema anaenda kumuita daktari, alivyosema anaenda kumuita daktari na
mimi nikaondoka nikiogopa anaweza akaamka akaanza kunipiga, niliondoka
nikawasha gari kuelekea Coco Beach kutuliza akili".
Muigizaji huyo ameendelea kusimulia kwamba ..."Nilivyofika Coco beach
meseji zilianza kusambaa kuniuliza kuwa nasikia Kanumba amefariki,
nikampigia 'Kidume' ambaye ni rafiki yake Kanumba kumuuliza Kanumba
yupo hospitali gani niende kumuona, akaniambia wewe usije hospitali,
niambie uko wapi, tukakubaliana tuonane Bamaga, tulivyokutana Bamaga
alikuwa kama anataka kuongea na mimi ghafla wakaja askari kunikamata".
Pamoja na hayo muigizaji huyo ameithibitishia mahakama kuwa alikuwa na
mahusiano ya kimapenzi na marehemu (Steven Kanumba) kwa muda wa miezi
minne kabla ya kukutwa na mauti.
Mahakama Kuu imeiahirisha kesi hiyo mpaka siku ya leo Oktoba 24, ambapo itasikilizwa tena
0 comments: