Mbunge
wa Chemba (CCM), Juma Nkamia, ameondoa kwa muda kusudio lake la kutaka
kuwasilisha muswada binafsi wa mabadiliko ya Katiba ya nchi ili kuongeza
ukomo wa ubunge.
Nkamia
aliwasilisha kusudio hilo Septemba, mwaka huu mjini Dodoma kwa mujibu
wa kanuni ya 81(2) ya kanuni za Bunge toleo la 2016, kupitia barua yake
aliyoisaini Septemba 12, mwaka huu iliyokuwa ikipendekeza kuongeza muda
wa Bunge kutoka miaka mitano hadi saba na kupunguza muda wa uongozi wa
vijiji kutoka miaka mitano hadi minne.
Kupitia
ujumbe mfupi aliouandika katika mtandao wa kijamii wa WhatsApp, Nkamia
alisema ameamua kuondoa kusudio hilo baada ya majadiliano na maelekezo
kutoka kwa viongozi wa juu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
“Ndugu
viongozi wenzangu, naomba kuwataarifu kuwa baada ya mashauriano na
maelekezo ya viongozi wa juu wa CCM na hali ya kisiasa katika nchi
kadhaa za Afrika Mashariki, nimelazimika kuondoa kwa muda hoja yangu
binafsi ya ukomo wa Bunge niliyokusudia kuiwasilisha katika Bunge lijalo
(linaloanza Novemba, mwaka huu,” aliandika Nkamia.
Hoja
ya Nkamia ilianzia Bunge lililopita lakini ilipingwa na wanasiasa
wakongwe akiwamo Spika Mstaafu wa Bunge, Pius Msekwa na wasomi
mbalimbali.
Akizungumza
na Kituo cha Televisheni cha Azam, Alhamisi wiki hii, Msekwa alisema
CCM haiwezi kukubaliana na maoni ya kuongeza muda wa kiongozi yeyote
kutoka kipindi cha miaka mitano kilichopo kwa mujibu wa Katiba ya sasa.
Pia
alisema kwa uzoefu wake bungeni anaona kuna tafakuri nyingi
zilizofanywa kabla ya Taifa kuamua kipindi cha utawala kuwa miaka mitano
na si vinginevyo.
Naye
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana,
alimpinga huku akisema lengo la Nkamia lilikuwa ni kujipendekeza kwa
Rais Dk. John Magufuli ili ampe uwaziri.
Pia
Septemba 18, mwaka huu, Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John
Heche, alisema anakusudia kuwasilisha bungeni hoja binafsi ili kupunguza
muda wa viongozi kukaa madarakani kutoka miaka mitano na iwe minne kama
Marekani ili kutoa nafasi kwa wananchi kuwa na uamuzi zaidi wa
kuendesha nchi yao.
0 comments: