TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA
WATOTO MHE. UMMY MWALIMU (MB) KUHUSU SIKU YA AFYA YA AKILI DUNIANI
TAREHE 10 OKTOBA 2017
Ndugu Wananchi,
Siku ya Afya ya Akili Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 10 ya Mwezi Oktoba.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya Afya ya Akili Duniani mwaka
2017 ni “Afya ya Akili Mahali pa Kazi” Kauli mbiu hii inalenga
kuhamasisha Waajiri na watunga sera namna bora ya kuhusisha Afya ya
Akili katika ngazi mbalimbali za kutengeneza miongozo ya kisera na
kuifanya afya bora ya akili kuwa ni sehemu ya ustawi wa wafanyakazi.
Ndugu Wananchi,
Tanzania kama ilivyo nchi zingine wanachama wa shirika la Afya
Duniani wanaadhimisha siku hii, ambapo Wizara ya Afya, Maendeleo ya
jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeandaa shughuli mbalimbali za kutoa
elimu kuhusu umuhimu wa afya ya akili mahali pa kazi na kuwafanya
waajiri na wafanyakazi kutambua umuhimu wa afya bora ya kiakili na
huduma za afya ya akili.
Ndugu Wananchi,
Tunapozungumzia afya tunamaanisha hali ya ustawi wa mwanadamu
kimwili, kiakili na kijamii. Mtu mwenye afya njema ya akili anaaminika
kwa kutengemaa katika namna anavyofikiri, anavyohisi, na anavyotambua
mambo, ambayo kwa pamoja hujionyesha katika matendo yake ya kila siku
ikiwa ni pamoja na jinsi anavyohusiana na kushirikiana na wenzake katika
familia na jamii na mahali pa kazi kwa ujumla.
Magonjwa ya akili ni magonjwa ambayo yanaathiri au yanapelekea
mabadiliko katika kufikiri, kuhisi, kutambua na kutenda, na hivyo kuwa
na mabadiliko ya kitabia au mwenendo uliotofauti au usioendana na jamii
husika kiimani, kimila, desturi, na nyanja nyingine za kijamii. Tabia
hizo zinatokana na ugonjwa wa akili kuathiri ufanisi na shughuli za mtu
husika (mgonjwa) pamoja na kuathiri uhusiano wake katika jamii na hivyo
huathiri jamii nzima inayomzunguka.
Visababishi vya magonjwa ya akili vimegawanyika katika sababu za
kibaolojia, kisaikolojia na kijamii na mjumuiko wa visababishi hivi
ndivyo vinavyopelekea mtu kuwa na dalili za ugonjwa wa akili.
Ndugu Wananchi,
Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni zinaonyesha kuwa kati ya watu
wazima wanne mmoja kati yao alishapata au alishaona mtu mwenye matatizo
ya kiakili, ambayo hutokana na mila na desturi zilizopitwa na wakati,
unyanyasaji, unyanyapaa na kutengwa au kubaguliwa kwa namna yeyote.
Hali kadhalika hata katika nchi yetu tumekuwa tukikabiliwa na
matatizo kama hayo ya mila na desturi zisizo rafiki, unyanyapaa na
ubaguzi ambao unasababisha pia ufinyu wa bajeti, uhaba wa wataalamu
katika vituo vya kutolea huduma, uhaba wa vifaa tiba na dawa kwa
wagonjwa wenye matatizo ya kiakili, kijamii na kisaikolojia.
Tunapaswa
kukumbuka kuwa hakuna afya njema ya kimwili kama hakuna afya ya akili;
na pia nchi yetu ikiwa na wafanyakazi wenye afya bora ya akili ni hazina
kubwa kwa Taifa letu.
Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na ukweli huu jitihada mbalimbali zimefanywa za
kutoa huduma za afya ya akili ikiwa ni pamoja na kutengeza Mwongozo wa
kisera wa afya ya akili ya mwaka, 2006 na Sheria ya Afya ya Akili ya
mwaka 2008 ambavyo unatoa mwongozo wa namna ya kutoa huduma.
Aidha,
serikali inaendelea kuhamasisha waajiri kuwekea mkazo mambo mbalimbali
ya kuimarisha huduma za afya ya akili katika mipango yao, na kuhakikisha
kila Mkoa unaimarisha huduma hizi katika ngazi ya Mikoa yote Tanzania
Bara.
Vilevile serikali inaendelea kuwajengea uwezo watoa huduma za afya ya
akili nchini ili waweze kutambua na kubaini mapema dalili za magonjwa
ya akili na kutoa matibabu stahiki au rufaa kwa wakati muafaka.
Pia,
tumeimarisha matibabu ya magonjwa ya akili na saikolojia katika
hospitali za mikoa na rufaa hii ikiwa ni pamoja na kupeleka wataalamu wa
afya ya akili wakiwepo madaktari bingwa na wauguzi bingwa ili kuweza
kutoa huduma kwa wagonjwa wa nje na wale wa ndani/ waliolazwa.
Ndugu Wananchi,
Watu wengi wamekuwa na uelewa mdogo kuhusu magonjwa ya akili, na
kufikia hatua ya kuhusisha na laana, kurogwa, kuwa na mapepo au kutupiwa
majini; Magonjwa ya akili ni magonjwa kama yalivyo mengine na yanaweza
kumtokea mtu yeyote wa rika lolote na muda wowote, hivyo basi wananchi,
wanafamilia na jamii kwa ujumla tunapaswa kujua na kutambua dalili za
magonjwa ya akili na kuwasaidia kupata matibabu, kupunguza unyanyasaji,
unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa wa akili. Taarifa ya afya na magonjwa
ya akili ya mwaka 2015/16 inaonyesha kuwa takribani wagonjwa 611,789
wameweza kuhudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma ya afya nchini.
Katika kukabiliana na wimbi la ugonjwa wa Afya ya akili wataalamu na
waajiri wataendelea kuelimisha jamii juu ya magonjwa ya akili na kupinga
vitendo vya unyanyasaji, unyanyapaa na kuwatenga wagonjwa hivyo,
kuwawezesha kufikishwa maeneo ya utolewaji wa huduma na tiba mapema ili
wasaidiwe kama walivyo wagonjwa wengine.
Ndugu Wananchi,
Dhamira kuu ya maadhimisho ya mwaka huu 2017, ni kuhakikisha afya ya
akili inakuwa sehemu ya agenda kila mwaka mahali pa kazi na kwamba
waajiri na waajiriwa waweze kuweka mikakati/mipango ambayo itazuia/
itapunguza au kuondoa visababishi vya magonjwa ya akili na uwezeshaji wa
utambuzi wa mapema kwa walio na dalili za magonjwa ya akili na hivyo
kupatiwa tiba.
Aidha, dhamira pia inalenga kuhakikisha kuwa mahali pa kazi ni mahala
salama na pasipokuwa na visababishi/vichochea/vihatarishi
vinavyopelekea waajiri na waajiriwa kupata dalili za magonjwa ya akili
kwa sababu ndio sehemu ambayo mwajiriwa/waajiriwa wanakaa muda mrefu
kuliko muda wa majumbani.
Vilevile, dhamira inalenga kuongeza thamani, heshima na utu wa
mgonjwa wa akili, kuzifanya huduma za afya ya akili kama sehemu muhimu
ya huduma ya mwili wa binadamu, kupunguza unyanyapaa, kutengwa na
kunyanyaswa, kuifanya jamii kuongeza uelewa na kutambua magonjwa ya
akili kama magonjwa mengine na hivyo kuyapa kipaumbele.
Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya ya mwaka (2007)
ambayo inalenga kutoa huduma bila malipo kwa wagonjwa wa akili na
magonjwa mengine yasiyoambukiza.
Aidha Sera ya Mwongozo wa Huduma za Afya ya Akili inasisitiza utoaji
wa huduma za Afya ya Akili bila malipo. Serikali kupitia Wizara ya
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kutambua
uwepo wa maadhimisho ya siku ya Afya ya Akili duniani kama sehemu ya
uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.
Ndugu Wananchi,
Ili kuboresha hali ya afya ya akili Serikali kwa kushirikiana na
wadau itahakikisha kwamba: – inaongeza uelewa wa jamii kuhusu
visababishi, dalili na huduma zinazohusiana na afya na magonjwa ya akili
ikiwemo:
- Watumishi wa afya wanapatiwa mafunzo maalum ya namna ya kuchujua/kuchunguza dalili za magonjwa ya akili na kutoa huduma stahiki kwa wagonjwa wa akili.
- Kufanya tafiti mbalimbali zinazosaidia kuboresha huduma za kuzuia na kudhibiti magonjwa ya akili katika jamii.
Tupe Maoni Yako( Matusi Hapana )
0 comments: