TUPINGE UBINAFSI TUNAPO MKUMBUKA BABA WA TAIFA
Na Joseph Yona
Ni miaka 18 sasa imepita tangu mzee wetu mpendwa baba wa taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aiage dunia.
Mwalimu Nyerere ni Rais wa kwanza na ni muasisi aliyeliletea taifa hili uhuru wa kweli toka katika makucha ya mkoloni 9 December, 1961.
Mwalimu Nyerere alizaliwa April 13, 1922 katika kijiji kidogo cha mwitongo huko Butihama, kasikazini mwa Tanzania karibu kabisa na ziwa Victoria . Alikuwa ni mtoto wa chifu Burito Nyerere wa kabila dogo la wazanaki
Nyerere alifariki dunia kwa ugonjwa wa kansa ya damu, siku ya Alhamisi Oktoba 14, 1999 saa 4:30 asubuhi [kwa saa za Afrika Mashariki], katika hospitali ya Mtakatifu Thomas London, Uingereza akiwa amezungukwa na timu ya madaktari bingwa.
Wakati wa uhai wake Mwalimu Nyerere alichukia na kukemea vikali mambo yasiyofaa kwa mustakabali wa maendeleo ya Tanzania , Afrika na Dunia kwa ujumla. Baadhi ya mambo hayo ni pamoja na ujinga.
Mwalimu Nyerere alikuwa ni miongoni mwa wasomi wachache na ni mtanzania wa kwanza kupata nafasi yamasomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Edinburg , Uingereza na kuhitimu mwaka 1952 akiwa ni gwiji wa uchumi na historia.
Mwalimu hakupenda ujinga na hivyo alipigana vita kali dhidi ya ujinga, na alifanikiwa kwa nafasi yake kuwaondoa ujinga watanzania wengi, wakiwemo viongozi wetu wa sasa ambao walisomeshwa bure katika mazingira mazuri yakuridhisha kwa manufaa ya nchi yetu.
Kama Nyerere asingechukia ujinga kwa kuboresha mazingira ya elimu, ikiwemo elimu ya watu wazima, basi leo hii tungekuwa na viongozi mazezeta'.
Ubinafsi, ambapo Mwalimu Nyerere aliaamini sana na kuyapa mkazo wa aina yake, ni pamoja na masuala ya haki na usawa. Mwalimu siku zote, alijenga imani katika misngi ya utu, haki na usawa kwa kila raia wa dunia hii.
Aidha Mwalimu alipinga sana mianya ya unyonyaji aliyoiita mirija'. Mwalimu alipinga sera zozote zinazoweza kuleta matabaka katika Taifa, iwe ni matabaka ya kiuchumi kwa kuwa na kundi la walionacho na wasionacho.
Mwalimu hakuruhusu ubinafsi na ufisadi ambao ambao leo hii umekithiri miongoni mwa viongozi wengi hapa nchini. Mwalimu aliwahi kusema "Hakuna mtu yeyote katika jamii atakayekuwa na mahitaji yote muhimu wakati wengine katika jamii hiyohiyo hawana chochote".
Mwalimu alijikita katika siasa ya ujamaa na kujitegemea na hatimaye Azimio la Arusha mwaka 1967, ili kahakisha keti ya Taifa inakuwa na mgawanyo sawa kwa wote.
Leo hii Azimio la Arusha limesahauika kabisa, hali ya viongozi wa serikali wanatanguza mbele maslahi binafsi hali ambayo baba wa Taifa aliipinga tabia hiyo chafu inayozidi kuchukua sura mpya kila kukicha.
Mwalimu alikuwa ni nuru ing'aayo gizani, alipinga mfumo wa ubepari kwa kuuita, mfumo wa ufukarishaji'. Hivyo aliimarisha misingi imara katika itikadi yake ya ujamaa na kujitegemea, ikiwa ndiyo itikadi pekee yenye misingi ya utu, haki na usawa ili kuondoa ubepari.
Mwalimu alichukizwa sana na mfumo mpya wa kibepari uliozuka baada ya yeye kung'atuka madarakani aliouita 'ubepari wa pembezoni' yaani ni ubepari wa kishenzi unaotoa mianya kwa wachache kutumia mirija kuwanyonya wanyonge.
Kuwezekana kwa jambo hilo, kutasaidia kuondoa taifa lenye watu linaloamini kujineemesha wao ndio fursa ya kuwa kiongozi na si kuwepo kwa kundi la watu linalofanya jitihada ya kuwakomboa wananchi kutoka kwenye lindi la umaskini walilokuwa nalo.
Hivyo, tunapaswa kumuenzi Mwalimu Nyerere kwa kuhakikisha tunaishi kwenye fikra zake, ambazo aliamini kiongozi anapaswa kuishi kwa kumtetea na kumlinda mwananchi ili aweze kunufaika na rasilimali zake, ambazo zitasaidia kumletea maendeleo.
About author: PAVEA BLOG
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
0 comments: