Tusimtupie Fundi SPANA Wakati Anakarabati Mtambo

Na mwandishi Maalumu, Mtanzania 
Nianze ‘Tafakuri Yangu’ kwa kukushirikisha usemi wa Kiingereza ninaoutafsiri kwa lugha yetu adhimu ya Kiswahili, kwamba mtambo au mashine inapoharibika fundi mkuu anapoikarabati baada ya kuifanyia tathmini, ndiye anayejua ilivyoharibika sanjari na aina na namba za spana zinazohitajika katika kuikarabati.

Kwa Kiingereza usemi: “Throwing spanners at works” ni nahau inayotumika kubainisha uvurugaji wa jambo linalokarabatiwa, kwamba kila anayedhani ni fundi zaidi ya anayekarabati hujiona anafaa kuliko aliyekasimiwa jukumu hilo, lakini heri mwenye mawazo kama hayo, kuna ambao humrushia fundi spana asizozihitaji kwa makusudi ili kuharibu lengo la kukarabati. Nadhani utakuwa umeelewa mashiko ya dhana hiyo inayoshadadia tukio adhimu lililotokea hivi karibuni, ambapo Rais Magufuli alitunuku vyeti wajumbe wa Kamati Maalumu za uchunguzi na majadiliano kuhusu rasilimali za nchi yetu.

Awali wakati mchakato umeanza kuhusu uthibiti wa makinikia, kisha baadaye dhahabu hata kutathmini upya sheria zetu zinazosimamia masuala ya madini jopo la mafundi lilianza kutupiwa spana na waliodhani ni mafundi zaidi ya waliokasimiwa kazi hiyo.

Mengi yalisemwa na kama isingekuwa ukimya na usiri wa kazi hiyo pengine hata hatua iliyofikiwa isingefikiwa ingawa pia ni kidato kimoja tu katika kuelekea kukamilisha mchakato kamili na kuzuia ‘utapia tija’ kwa jisi tulivyokuwa hatufaidiki na rasilimali tulizokirimiwa na mwenyezi Mungu.

Hata sasa pamoja na kwamba hatua imefikiwa katika suala hilo chapuo kubwa limeanza kupigwa kwa kushabikia zaidi kutupisha spana kwenye baadhi ya makubaliano ikiwemo fidia ya dola milioni 300. Ukiachana na hulka za watupishaji spana kuna mambo ya msingi yamefanyika na kubadili mwelekeo kutoka mdororo na kuzuia mporomoko wa upatikanaji tija, kuelekea hali chanya kwamba badala sasa ya sisi kusalia na asilimia tano tu ya madini ambayo hayapatikani kokote duniani isipokuwa hapa kwetu ndiyo maana yanaitwa ‘Tanzanite’ tutajizolea asilimia tisini na tano.

Hii inanikumbusha usemi kwamba maisha ni sawa na kupanga mstari mkiambiwa geukeni nyuma wa mbele atakuwa nyuma na wa mwisho atakuwa wa mbele, hii ndiyo ile ya kibao kugeuka ghafla japo hiki tulikigeuza baada ya kustukia kuwa tunaibiwa.

Fundi mkuu (Rais Magufuli) aliifanya kazi hiyo kwa mchakato wa kujiamini ndiyo maana tumefikia tulipo sasa katika suala hilo, ingawa spana nyingine alizotupishiwa yeye mwenyewe binafsi na kamati alizoziteua alifafanua kwamba zilisababisha mtikisiko mkubwa ambao yeye mwenyewe anafahamu namna ulivyomtesa ingawa kwa kuwa aliamini analolifanya ni sahihi basi aliamua kukomaa liwalo na liwe.

Kitakachopatikana ni kwa faida ya vizazi vya sasa na vijavyo kwa maslahi ya Tanzania ambayo kila mmoja wetu anazaliwa ndani yake lakini anaiacha anapofarikiana na dunia.

Nadhani kwenye mafanikio hayo spana hazitarushwa tena japokuwa bado kuna hali ya kurusha kwa bezo, kwamba kuna yaliyokubaliwa ambayo hayawezi kutekelezeka kama taarifa za Acacia iliyoko chini ya Barrick Gold kudai kuwa haina uwezo wa kulipa dola ambazo kampuni mama inayoisimamia kampuni hiyo tanzu imekubali kufanya hivyo. Kwa hili lililotimizwa ‘Tafakuri Yangu’ inalipa Kongole kwani litaongeza mapato na hatutafanya tu kwa kiwango cha miradi inayoendelea sasa, mathalan, ujenzi wa barabara na elimu bure lakini pia ununuzi wa meli na uimarishaji mfumo wetu wa umeme kwa kutangaza kandarasi ya bwawa kubwa la kufua umeme la Strigler’s Gorge pamoja na ujengaji wa Reli ya kisasa na usambazaji umeme vijijini bali tutafanya zaidi.

Ingawa matumaini ni makubwa kwa hatua tuliyofikia lakini safari bado inaendelea kwani kuna mengi tunayopaswa kuyapata, kwa kuwaacha mafundi wataje spana zinazohitajika katika kukarabati mfumo ingawaje nao pia wanapaswa kuzingatia taarifa za wadau, ambao mfumo haukuwa ukiwatendea haki wakiwemo wananchi na viongozi pinzani wa siasa.

Ni katika maudhui ya ujenzi wa nyumba moja bila kugombea fito kama tunadhamiria vizazi vijavyo vifaidi matunda ya uhuru kama kauli mbiu za miaka ya mwanzoni zilivyobainisha kuwa: ‘Uhuru ni kazi’ na baadaye kubadilishwa kidogo na kuwa: ‘Uhuru na kazi’ na hakika maendeleo hayatakuja kwa kuruhusu rasilimali kutokomea kwa kuchukuliwa kirahisi kutokana na makosa ya kiutendaji kwa mikataba mibovu.

Hata hivyo kila wingu jeusi lina upapi wa mn’garo wa fedha kama ambavyo baada ya kuwekwa wazi mabadiliko ya nafasi ya juu ya BOT tashwishwi nyingi zinazowakereketa wahafidhina wa tija ya nchi yetu, zimepelekea wabainishe vipaumbele vya kugudua vimeo ambavyo kutokana na usimamizi duni vinatatanisha mfumo wetu wa fedha ikiwemo utakatishaji fedha, kulinda mfumo wa mzunguko wa fedha ili kuimarisha thamani ya shilingi yetu isidorore zaidi na ushirikishwaji wa sekta rasmi na binafsi katika ujenzi wa uchumi. Ushauri kama huu ndiyo spana anazohitaji fundi sio anazotupishiwa!
Share on Google Plus

0 comments: