CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeliandikia
Bunge la Tanzania kuliarifu kwamba Mbunge wa Singida Kaskazini, Lazaro
Nyalandu amepoteza sifa za kuwa mwanachama wake, siku chache baada ya
mbunge huyo kutangaza kuwa amejiuzulu nyadhifa zake zote katika chama
tawala.
Kwa hatua hiyo, Ofisi ya Spika wa Bunge
la Tanzania, Nyalandu aliyewahi kuwa Waziri katika Serikali ya Awamu ya
Nne, amepoteza sifa ya kuwa mbunge. Hayo yamebainishwa kwenye taarifa
iliyotolewa jana na Ofisi ya Spika ikithibitisha kupokea barua ya CCM
iliyotumwa kwenye ofisi hiyo Oktoba 30, mwaka huu. Kwa mujibu wa taarifa
hiyo, Nyalandu amevuliwa ubunge huo baada ya kupokea barua kutoka CCM
ikiiarifu Ofisi ya Spika kuwa amekosa sifa za kuwa mwanachama wa CCM.
Barua ya CCM iliyoandikwa na Katibu Mkuu
wa chama, Abdulrahman Kinana kwenda Ofisi ya Spika ilibainisha kuwa kwa
muda sasa chama hicho kilishaanza kumchukulia Nyalandu hatua za
kiudhibiti na kinidhamu dhidi ya vitendo na kauli zake zisizoridhisha
kinyume cha msingi, falsafa na itikadi ya chama hicho.
“Hivyo, Chama Cha Mapinduzi kuanzia
tarehe ya barua yao kimemjulisha Mheshimiwa Spika kuwa Ndugu Lazaro
Nyalandu amepoteza sifa za uanachama wa Chama Cha Mapinduzi, na hivyo
kupoteza nafasi zote za uongozi wa ndani wa chama hicho na ubunge kwa
mujibu wa Ibara ya 13 ya chama hicho,” ilieleza taarifa ya ofisi ya
Spika.
Kutokana na kupokea barua ya CCM, ofisi
ya Spika ilibainisha kuwa, kutokana na Ibara ya 71(1) (e) ya Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nyalandu si mbunge tena. Kwa mujibu wa
Ibara ya 71(1) (e) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ‘Mbunge
atakoma kuwa Mbunge na ataacha kiti chake cha Ubunge iwapo litatokea
lolote kati ya mambo yafuatayo: (e) iwapo Mbunge ataacha kuwa mwanachama
cha chama alichokuwamo wakati alipochaguliwa au alipoteuliwa kuwa
Mbunge.”
“Mheshimiwa Spika, angependa kuwaarifu
Watanzania kwamba, kwa barua hiyo kutoka mamlaka halali ndani ya Chama
Cha Mapinduzi ambacho Ndugu Lazaro Nyalandu alipata Ubunge na kwa mujibu
wa Ibara ya 71(1) (f) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Lazaro Nyalandu si mbunge tena na hatua stahiki za kuiarifu Tume ya
Taifa ya Uchaguzi zinaendelea kuchukuliwa,” ilifafanua taarifa hiyo.
Aidha, Ofisi ya Spika ilizidi kubainisha
kuwa mpaka jana ilikuwa haijapokea barua ya Nyalandu ya kujiuzulu
ubunge. “Ofisi ya Spika inapenda kuwaarifu kwamba mpaka sasa (jana)
haijapokea barua kutoka kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Singida
Kasikazini (CCM), Lazaro Nyalandu ambayo amekuwa akiarifu kwamba
amemwandikia Spika kumtaafiru kujiuzulu wake,” alibainisha.
Jumatatu wiki hii akiwa jijini Arusha,
Nyalandu aliyekuwa Waziri wa Maliasili na Utalii wakati wa Serikali ya
Awamu ya Nne na aliyejitosa kuwania Urais wa Tanzania kupitia chama
hicho tawala, alitangaza kujiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya CCM
ikiwemo ubunge. Nyalandu alidai amechukua uamuzi huo kutokana na
kutokuridhishwa na mwenendo wa sasa wa siasa, ukiukwaji wa haki za
kibinadamu na kutokuwepo kwa mipaka baina ya mihimili ya dola- Serikali,
Bunge na Mahakama.
Chanzo-Habarileo
0 comments: