Mbunge wa CUF Ashinda Pingamizi la Serikali Mahakamani

Mbunge wa Malindi (CUF), Ally Saleh ameruka kihunzi cha Serikali mahakamani, baada ya kushinda pingamizi la awali lililowekwa na Serikali katika kesi ya kuhoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi ya wadhamini wa chama hicho.

Saleh ambaye pia ni mwanasheria amefungua kesi Mahakama Kuu akihoji uhalali wa wajumbe wapya wa bodi waliosajiliwa na Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita).

CUF imegawanyika pande mbili; inayomuunga mkono Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad na inayomuunga  Mwenyekiti, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, ambaye ndiye aliunda bodi inayopingwa.

Wadaiwa katika kesi hiyo ni Ofisa Mtendaji wa Rita, anayewakilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kupitia jopo la mawakili wa Serikali linaloongozwa na Gabriel Malata.

Wengine ni bodi ya wadhamini (mpya) ya CUF, mwenyekiti wa bodi hiyo, Peter Malebo, wanaowakilishwa na wakili Majura Magafu na wajumbe wapya wa  bodi hiyo wanaowakilishwa na wakili Mashaka Ngole.

Wadaiwa wengine ni wajumbe wa bodi waliomaliza muda wao na ambao wengine walipendekezwa tena na upande wa Maalim Seif ambao hata hivyo hawakuidhinishwa na Rita, wanaowakilishwa na mawakili Juma Nassoro, Daimu Halfan na Hashim Mziray.

Serikali kwa niaba ya mdaiwa wa kwanza (Mtendaji wa Rita), iliweka pingamizi la awali ikiiomba Mahakama iitupilie mbali kesi, ikitoa hoja kuwa imefunguliwa kabla ya wakati bila kufuata utaratibu wa kuishtaki Serikali na kwamba mdai amemshtaki mtu asiyestahili.

Saleh anayewakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Fatma Karume, ameshinda pingamizi hilo katika uamuzi uliotolewa na Jaji Wilfred Dyansobera alioutoa jana Jumatano, Novemba 29,2017.

Jaji Dyansobera ametupilia mbali pingamizi hilo la Serikali baada ya kuridhika kuwa hoja za pingamizi hilo hazikuwa na mashiko.

Wakati wa usikilizwaji wa pingamizi hilo, wakili Malata alidai mdai amemshtaki mtu asiye sahihi; akidai Rita ni wakala ndani ya ofisi ya Kabidhi Wasihi Mkuu ambaye ndiye aliyestahili kushtakiwa na si mtendaji wa Rita.

Pia, alidai kesi ilifunguliwa kabla ya wakati kwa kuwa ilifunguliwa kabla ya kutoa taarifa ya kusudio kwa Serikali ya siku 90, kama inavyoelekezwa katika sheria ya mashauri dhidi ya Serikali.

Wakili Mpoki alipinga hoja hizo akidai mtu waliyemshtaki ni sahihi na kwamba, kwa aina ya kesi hiyo hapakuwa na haja ya kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa hawaishtaki Serikali.

Jaji Dyansobera katika uamuzi wake amekubali hoja za upande wa mdai, kuwa suala la nani ashtakiwe na nani asishtakiwe ni jukumu la mdai kwa kuwa ndiye anaona kuwa nafuu anazoziomba atazipata kwa nani.

Amesema kesi hiyo haikuhitaji kutoa taarifa ya siku 90 kwa Serikali kwa kuwa si Serikali inayoshtakiwa bali kesi hiyo inahusu mgogoro wa ndani ya chama cha siasa, ambako Serikali haipaswi kujiingiza wala kuwa na upande.

Jaji Dyansobera amepanga kuendelea na usikilizwaji wa kesi hiyo Desemba 8,2017 kwa kusikiliza hoja za msingi za mbunge Saleh na majibu ya wadaiwa na kisha atapanga tarehe ya kutoa uamuzi.
Share on Google Plus

0 comments: