Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),
Mhe. Selemani S. Jafo (Mb), ameiagiza Mikoa yote nchini kuanza mapema
maandalizi ya kuwapokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka 2018,
kufuatia kuongezeka kwa ufaulu.
Mhe.
Jafo ametoa kauli hiyo mjini Dodoma, wakati akiongea na Waandishi wa
Habari, juu ya kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi watakaojiunga na kidato
cha kwanza mwaka, 2018,
“Wakuu
wa Mikoa hakikisheni miundombinu iliyopo inatosha katika mikoa yenu ili
watoto wote waliofaulu, wapate nafasi ya kujiunga na kidato cha kwanza
hapo Januari, 2018”, ameitaja mikoa ya Dar es Salaam, Geita, Kagera,
Njombe, Tanga, Morogoro, Lindi, Rukwa, Pwani, Mtwara na Songwe kuwa na
idadi kubwa zaidi na hivyo maandalizi ya madarasa, vyoo na madawati
yatahitajika kwa kiwango kikubwa.
Aidha,
amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa, kusimamia zoezi la uchaguzi wa
wanafunzi tarajiwa wa kidato cha kwanza ili ifikapo Desemaba 8, 2017
wawe wamekwisha tangaza.
Mhe.
Jafo ameagiza kufanyika uchambuzi ili kubaini sababu zilizopelekea
watahiniwa zaidi ya asilimia moja kutofanya mitihani katika mikoa ya
Geita, Katavi, Mara, Rukwa, Songwe, Dodoma na Manyara kwa lengo la
kuondoa mdondoko wa wanafunzi kutoka ngazi moja hadi nyingine.
Pia
amezitaka Halmashauri zilizopata ufaulu chini ya asilimia hamsini
kujiwekea mikakati ya kupandisha ufaulu wa wanafunzi, Halmashauri hizo
ni pamoja na Mkalama, Meatu na Simanjiro.
Matokeo
ya darasa la saba, yalitangazwa rasmi hivi karibuni, ambapo jumla ya
watahiniwa wapatao 662,035 walifaulu kwa kupata madaraja ya A, B na C,
ikiwa ni sawa na asilimia 72.76 ya watahiniwa wote.
Ofisi
ya Rais TAMISEMI, yenye dhamana na usimamizi wa Elimu ya Awali, Msingi
na Sekondari imechukua hatua za makusudi, ili kupunguza au kuondoa
wanafunzi waliofaulu mtihani wa darasa la saba kutopangiwa shule na
kujiunga na kidato cha kwanza mwaka, 2018.
0 comments: