Naibu
Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewaagiza watendaji wa Tanesco
kuhakikisha kuwa hawakati Umeme bila sababu maalum na hivyo kuwaondolea
wananchi adha ya kukosa nishati hiyo.
Naibu
Waziri aliyasema hayo wakati wa ziara yake ya kukagua mradi wa TEDAP
unaohusu upanuzi na ujenzi wa vituo vya kupozea Umeme na njia za Umeme
ambapo vituo vya kupozea Umeme alivyovitembelea ni Mbagala, Gongo la
Mboto, Kipawa na City Centre.
“Umeme
ukatike pale inapostahili tu, na endapo tatizo linatokea mfano kwenye
mifumo ya Umeme ni muhimu mkatoa taarifa mapema kwa wananchi,” alisema
Subira Mgalu.
Aliongeza
kuwa ukatikaji wa Umeme unasababisha malalamiko kutoka kwa Wananchi
kwani kukosekana kwa nishati hiyo kunaathiri shughuli nyingi hasa za
kimaendeleo na kiuchumi zinazowaingizia kipato.
Aidha
Naibu Waziri aliwaagiza watendaji wa TANESCO wanaosimamia mradi huo wa
TEDAP jijini Dar es Salaam, kuhakikisha kuwa kazi hiyo inakamilika
tarehe 15 Desemba, 2017.
Vilevile
alieleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo unaendelea vizuri na kwamba
kukamilika kwake kutaboresha hali ya upatikanaji wa Umeme katika jiji la
Dar es Salaam.
“Nawaomba
watanzania wawe na matumaini na Serikali ya Awamu ya Tano kwani
inajitahidi katika Ujenzi wa miundombinu ya Umeme, nia ikiwa ni nishati
ya Umeme kupatikana muda wote,” alisema Naibu Waziri.
kwa
upande wake, Meneja Mradi wa Usafirishaji na Usambazaji Umeme kutoka
TANESCO, Mhandisi Emmanuel Manirabona alisema kuwa Shirika hilo
linafanya juhudi mbalimbali ili utekelezaji wa mradi huo ukamilike ndani
ya muda ulioelekezwa.
Mradi
wa TEDAP unahusisha upanuzi na ujenzi wa Vituo Vipya 19 vya kupoza
Umeme wa Msongo wa kV 132/33 na kV 33/11 pamoja na ujenzi wa njia za
Umeme wenye Msongo wa kV 132, kV 33 na kV 11 katika Mikoa ya Arusha, Dar
es Salaam na Kilimanjaro.
Gharama
za utekelezaji wa mradi husika ni Dola za Marekani milioni 43, ambazo
zimetolewa na Benki ya Dunia (WB) kupitia Mradi huo.
0 comments: