Imeelezwa
kuwa ujenzi wa mitambo ya kuzalisha Umeme wa kiasi cha megawati 240 kwa
kutumia Gesi Asilia katika mradi wa Kinyerezi II umefikia asilimia 84.
Hayo
yameelezwa jijini Dar es Salaam na Meneja Miradi ya Umeme ya Kinyerezi,
Mhandisi Stephen Manda wakati akitoa taarifa ya miradi ya Kinyerezi I
(MW 150), Kinyerezi I-Extension (MW 185) na Kinyerezi II (MW 240) kwa
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu.
Naibu
Waziri Mgalu alifanya ziara katika mitambo hiyo lengo likiwa ni kupata
taarifa na kukagua kazi iliyofanywa na Wataalam wa TANESCO ya kusafisha
na kuunga Bomba kubwa la Gesi katika mitambo ya Kinyerezi I iliyofanyika
Novemba 18 na 19 mwaka huu na hivyo kusababisha upungufu wa Umeme
katika gridi ya Taifa.
Akitoa
taarifa ya utekelezaji wa shughuli hiyo, Mhandisi Manda alieleza kuwa
TANESCO walikamilisha zoezi hilo kwa ufanisi na ilipofika mchana wa
Novemba 20, 2017 mitambo hiyo iliingiza megawati 115 katika Gridi ya
Taifa na hivyo kuboresha hali ya upatikanaji wa Umeme.
Kuhusu
mradi wa Kinyerezi II unaotekelezwa na Mkandarasi SUMITOMO kutoka
nchini Japan, Mhandisi Manda alisema kuwa matarajio ni kuanza kuzalisha
Umeme mwanzoni mwa mwezi Disemba mwaka huu ambapo megawati 30 zitaanza
kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Aidha,
alisema kuwa, matarajio ni mitambo hiyo kuongeza megawati 30 kwenye
gridi ya Taifa kila mwezi mpaka zitakapokamilika megawati 240 mwezi
Julai, 2018.
Alieleza
kuwa, Mkandarasi wa mradi huo anatarajia kukabidhi mradi husika kwa
Serikali Septemba 30, mwaka 2018 na kuongeza kuwa Wataalam wazawa
watakaoendesha kituo hicho tayari wamepata mafunzo kutoka nje na ndani
ya nchi.
Kuhusu
utekelezaji wa mradi wa Kinyerezi I-Extension (MW 185), alisema kuwa
utekelezaji wake umefikia asilimia 48 na kwamba ujenzi wa misingi yote
ya mitambo na viambata vyake imekamilika.
Aliongeza
kuwa, mitambo yote ya Umeme itakayotumika kwenye mradi huo
imeshatengenezwa na ipo tayari kuletwa nchini baada ya kukaguliwa na
wataalam na kwamba Wataalam wa TANESCO wapo nchini Norway kwa ajili ya
kukagua mifumo ya uendeshaji wa mitambo hiyo kabla kusafirishwa kuja
nchini.
kwa
upande wake Naibu Waziri wa Nishati aliwapongeza wataalam wa TANESCO
kwa kusimamia kwa umakini miradi hiyo na kuwataka kuendelea kufanya kazi
usiku na mchana ili kuweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
0 comments: