Tanzania imeiomba Mahakama ya Jimbo la Columbia kutupilia mbali ombi la Stirling Civil Engineering la kutaka kusajili hukumu mbili za Mahakama ya Kimataifa Usuluhishi ili kampuni hiyo ya Uingereza ikamate mali nyingine za Serikali zilizopo nchini Marekani.
Stirling, ambayo ni kampuni ya ujenzi iliyokatishwa zabuni ya kujenga Barabara ya Bagamoyo kutoka eneo la Wazo Hill kutokana na kutekeleza mradi huo chini ya kiwango, ilishinda ksi iliyofungua kupinga kitendo hicho msuluhishi akaagiza ilipwe dola 38 milioni za Kimarekani.
Kampuni hiyo ilisajili uamuzi huo wa msuluhishi nchini Uingereza na Uholanzi na kufanikiwa kushikilia ndege aina ya Bombardier Q400 iliyonunuliwa na Serikali na sasa inataka mahakama isajili hukumu mbili za mwaka 2015 na 2016 zisajiliwe Marekani ili ipate nguvu ya kushikilia mali nyingine.
Lakini Serikali ya Tanzania imeamua kupambana na kampuni hiyo mahakamani kuizuia isiendelee kukamata mali zake.
Kwa mujibu wa tovuti ya Law360, ambayo ni maalum kwa ajili ya habari za kisheria, Tanzania imewasilisha pingamizi, ikitaka mahakama hiyo isisajili hukumu hiyo ya Mahakama ya Kimataifa ya usuluhishi.
Katika hoja yake, Tanzania imesema mahakama hiyo haina mamlaka ya kisheria ya kushughulikia ombi hilo la Stirling.
Serikali inasema ina kinga dhidi ya hukumu mbili zilizotolewa na mahakamani nchini Uingereza na Uholanzi ambazo kampuni hiyo inaomba zitambuliwe pia Marekani, ikisema kuwa ondoleo hilo la kinga linalotolewa na Sheria ya Kinga ya Mataifa ya Kigeni, haiwezi kutumika.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, Sheria ya Kinga ya Mataifa ya Kigeni inasema taifa la kigeni halitakuwa na kinga dhidi ya mamlaka ya mahakama ya Marekani katika mashauri yanayowasilishwa kwa ajili ya kuthibitisha tuzo za mahakama ya usuluhishi zinazoongozwa na makubaliano yaliyoidhinishwa na nchi yanayotambuliwa nchini Marekani.
Serikaloi inasema Stirling inataka kutambuliwa kwa hukumu za mahakama ya nje ili ziwe na nguvu, badala ya kuomba kutekelezwa kwa hukumu hizo.
“Kuna tofauti inayotambulika vizuri kati ya kuthibitisha tuzo ya msuluhishi, kwa upande mmoja, na kutambua hukumu ya mahakama ya nje, kwa upande mwingine,” tovuti hiyo inakariri hoja hizo za Serikali.
“ingawa tuzo ya msuluhishi na hukumu ya mahakama zinalingana kwa kiasi kikubwa, hata hivyo zina tofautiana.”
Kwa hiyo, Serikali inasema Stirling haiwezi kutumia mwanya huo, kuomba utekelezaji wa hukumu hizo.
Kampuni hiyo inadai kuwa kitendo cha Serikali ya Tanzania kukubali kwenda kwenye Mahakama ya Usuluhishi, kiliondoa kinga hiyo na kuipa yenyewe haki ya kulipwa fidia hiyo.
Mwaka 1999 Serikali iliipa kandarasi kampuni ya Impresa Ing. Fortunato Federici SpA (IFF) ambayo baadaye ilinunuliwa na Stirling, kukarabati barabara ya Wazo Hill-Bagamoyo, lakini baadaye ikatimuliwa.
Mwaka 2004 kampuni hiyo ilifungua kesi Mahakama ya Usuluhishi wa Kimataifa na hukumu ilitolewa mwaka 2009 na 2010, lakini Serikali haikulipa fidia iliyopendekezwa na kuilazimu kukazia hukumu Uingereza na Uholanzi.
Novemba 2015, mahakama nchini Uingereza iliridhia utekelezaji wa hukumu hiyo na Uholanzi ilifanya hivyo Desemba 2016.
0 comments: