Dares Salaam, Novemba 14, 2017:
Sweden imeipatia Tanzania Msaada wa jumla ya Fedha ya Sweden SEK.
Bilioni 1.64 ambayo ni sawa na takribani Sh. bilioni 435.79 kwa ajili ya
Msaada wa kibajeti na kusaidia mpango wa elimu.
Makubaliano
ya msaada huo yamesainiwa Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu
Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James na Mkuu wa Kitengo cha
Ushirikiano na Maendeleo wa Ubalozi wa Sweden nchini Tanzania Bw. Ulf
Kallsting.
Bw.
James alisema kuwa imesainiwa Mikataba mitatu ya msaada huo ambayo ni;
mkataba kwa ajili kusaidia Bajeti ya Serikali wa kiasi cha SEK milioni
600 ambazo ni sawa na Sh. bilioni 159.59 kwa kipindi cha kuanzia mwaka
2017/18 hadi 2019/2020, ambapo kwa mwaka wa fedha 2017/2018 watatoa
takribani Sh. bilioni 53.20.
Alisema
fedha hizo zitaelekezwa katika kuboresha uhalisia wa Bajeti ili kuweza
kutimiza majukumu ya kisera, kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya
kikodi na yasiyo ya kodi na pia kusaidia Serikali kutoa huduma nzuri
kwa wananchi kupitia taratibu za manunuzi.
Mkataba
mwingine ni kwa ajili ya kusaidia Mpango wa Elimu kwa Matokeo (EPforR)
wa kiasi cha Fedha ya Sweden SEK milioni 885 ambayo ni sawa na Sh.
bilioni 235.40 kuanzia mwaka 2017/18 hadi 2020/2021.
“Lengo
la msaada huu ni kusaidia Mpango wa Elimu kwa Matokeo ambapo tunapimwa
namna ambavyo tumeweza kutimiza wajibu wetu tuliojiwekea katika bajeti.
Baada ya ya Serikali kutimiza wajibu wake wa kupeleka fedha katika Sekta
ya Elimu kwa wakati, wameamua kutupatia fedha hizo ambazo Serikali
tunazipangia kazi kulingana na vipaumbele”, alieleza Bw. James.
Alieleza
kuwa Mpango wa Elimu kwa Matokeo ulianza mwaka 2015/ 2016 na katika
kipindi hicho yamepatikana maendeleo makubwa katika ujenzi wa
miundombinu ya madarasa, vyoo, mabweni. Utekelezaji wake umefanywa
katika shule 361 kwenye Halmashauri 129 nchini.
“Katika
Mpango huo Vyuo 17 vya Walimu vimekarabatiwa ikiwa ni pamoja na kununua
Kompyuta 260, Magodoro 6,730 na viti 1,976. Mpango huu unafanikiwa
kutokana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kuweka mkazo katika
Sekta ya Elimu hivyo kupeleka fedha kwa wakati jambo linalosababisha
washirika wa maendeleo wazidi kutuamini” alifafanua Bw. James.
Mkataba
wa tatu ni Marekebisho ya Mkataba wa Mpango wa Kusoma, Kuhesabu na
Kuandika ambao una kiasi cha Dola za Marekani 94.8 zilizotolewa na
Taasisi ya Kimataifa ya Global Partnership for Education (GEP) na
kukabidhiwa kwa nchi ya Sweden ili iweze kuusimamia.
Akifafanua
kuhusu Mkataba huo Bw. Doto James alisema kuwa Serikali ili saini
Mkataba huo na Sweden Mei, 2015 na muda wa utoaji wa fedha hizo
ulikwisha Agosti, 2016 na kubakia kiasi cha Dola milioni 18.3 ambazo
zitapatikana baada ya kusainiwa kwa mkataba huo.
Kwa
upande wake Mkuu wa Kitengo cha Ushirikiano na Maendeleo katika Ubalozi
wa Sweden nchini Tanzania Bw. Ulf Kallsting amesema kuwa nchi yake
imedhamiria kuhakikisha inajenga uwezo na ujuzi kwa watanzania kuanzia
elimu ya Awali kwa kuwa nchi yake inathamini sana elimu.
Bw.
Kallsting alisema kuwa Tanzania imekuwa na uhusiano mzuri na Sweden na
inatekeleza kwa ufanisi miradi mbalimbali hivyo nchi yake itaendelea
kuisaidia Tanzania katika maeneo mbalimbali ya Maendeleo ili kufanikisha
mipango yake.
Katibu
Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Doto James ameishukuru Sweden kwa
niaba ya Serikali kwa kuendelea kuisaidia Tanzania katika kutekeleza
bajeti yake.
Imetolewa na;
Benny Mwaipaja
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini
Wizara ya Fedha na Mipango
0 comments: