SIASA ZA KENYA: Balozi wa Kenya nchini Tanzania Chirau Mwakwere ajiuzulu


http://ichef-1.bbci.co.uk/news/660/cpsprodpb/16988/production/_94625529_97cddfec-0537-41df-8a6b-af4247ecf14f.jpgRais mstaafu wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete na Bw Chirau Ali Mwakwere Februari 2015. 


Balozi wa Kenya nchini Tanzania Chirau Ali Mwakwere amejiuzulu.
Bw Mwakwere, ambaye amekuwa balozi wa Kenya katika nchi hiyo jirani tangu mwanzoni mwa mwaka 2015, alijiuzulu rasmi Ijumaa kumuwezesha kuwania katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Agosti mwaka huu.

Watumishi wa umma kikatiba wanafaa kujiuzulu kufikia 15 Februari.
Bw Mwakwere, ambaye mwishoni mwa wiki alitangaza rasmi kuhamia chama cha upinzani cha ODM, alikuwa awali mwanachama wa chama cha URP, moja ya vyama vilivyounda muungano wa Jubilee ulioshinda uchaguzi mkuu mwaka 2013.
Aliwania wadhifa wa seneta katika uchaguzi huo lakini akashindwa na Boy Juma Boy wa chama cha ODM.

Bw Mwakwere ni miongoni mwa waliotangaza nia ya kuwania wadhifa wa ugavana katika kaunti ya Kwale, baada ya gavana wa sasa Salim Mvurya kuhama chama cha ODM na kujiunga na chama Jubilee chake Rais Uhuru Kenyatta na Naibu Rais William Ruto.
"Nimekuwa balozi, wadhifa muhimu sana wa kutumikia maslahi ya wananchi wa Kenya katika ngazi ya kibalozi. Kazi yangu sasa ni kuimarisha hali ya maisha ya watu wa Kwale," alisema Jumapili, kwa mujibu wa gazeti la Daily Nation la Kenya.

"Ninataka kuweka mambo wazi, nimejiondoa chama cha Jubilee na sasa niko na watu wangu katika National Super Alliance (muungano wa wagombea wa upinzani."
Mwakwere, 71, alihudumu kama waziri wa mambo ya nje wa Kenya kati ya 2004 na 2005 na baadaye akateuliwa waziri wa uchukuzi Desemba 2005.

Alipoteza wadhifa wake wa uwaziri Februari 2010 baada ya kushindwa katika kesi ya kupinga kuchaguliwa kwake kama mbunge wa Matuga lakini alishinda uchaguzi wa marudio baadaye mwaka huo dhidi ya mpinzani wake Hassan Mwanyoha.
Share on Google Plus

0 comments: