BALOZI SEIF ALI IDD AONGOZA MAZISHI YA ALIYEKUWA KATIBU WA CCM WILAYA YA KUSINI UNGUJA MAREHEMU HAMDANI



index
NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR.
MJUMBE wa Kamati kuu ya CCM, Balozi Seif Ali Idd ameongoza mamia ya wanachama wa Chama na Wananchi kwa ujumla katika mazishi ya  aliyekuwa Katibu wa CCM Wilaya ya Kusini Unguja Marehemu Hamdani Haji Machano aliyefariki ghafla jana kwa maradhi ya baridi.

Maziko hayo yamefanyika  katika kijiji cha Donge Shehia ya Mtambile Mkoa wa Kaskazini Unguja, na kuudhuriwa na wananchi  pamoja na baadhi ya  wajumbe wa kamati kuu, Halmashauri kuu za CCM, Wenyeviti , Makatibu wa Mikoa na Wilaya,  Wakuu wa Mikoa na Wilaya za Zanzibar pamoja na Wajumbe wa NEC.

Akizungumza mara baada ya maziko hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar  Dkt.Abdalla Juma Saadalla “Mabodi ”  alisema Chama hicho kimepokea kwa mshituko na masikitiko  makubwa taarifa ya kifo cha Mtendaji huyo na kuwaomba wanafamilia, ndugu na jamaa kuwa na subira katika kipindi hiki cha msiba.

Ameeleza kwamba marehemu Hamdani alikuwa ni  Kiongozi mwadilifu na mchapakazi na aliyekuwa akijitolea kufanya kazi kwa bidii huku akisimamia kwa dhati maslahi ya Chama hicho.
Dkt.Mabodi alifafanua kwamba kutokana na mchango mkubwa uliotolewa na marehemu huyo wakati wa Utumishi wake, CCM itaendelea kuenzi juhudi hizo kwa kusimamia mamlaka za kiutendaji ndani ya chama na serikali ili ziendelee kutenda haki kwa wananchi wote.

“Tumepokea kwa mshituko mkubwa kifo cha Mtendaji mwenzetu na hili ni pengo kubwa linalotakiwa kuzibwa na umoja wetu katika na kukitumikia chama chetu kwa uzalendo ili kishinde kila uchaguzi na kuendelea kuongoza dola kusimamia yote mazuri yaliyoachwa na Marehemu Hamdani.

Pia nakumbuka hivi juzi tu katika ziara zangu tulikuwa pamoka katika Mkoa wake wa kazi tukishauriana mambo mengi ya Kiutendaji na kisiasa, naomba Mwenyezi Mungu amjaalie mapumziko mema na yenye kheri na yeye Amin.”, alieleza Dkt.Shein.

Kwa upande wake Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka aliweka bayana kwamba Marehemu Hamdani alisema kwamba ni kada wa kweli yaliyepigana kuona  CCM na Jumuiya zake zinapiga hatua kubwa kimaendeleo.

Naye Mkaazi wa Shehi ya Chanjaani, Masoud Haji Choum alisema mbali na Marehemu huyo kuwa na ushirikiano mzuri na viongozi wa chama na serikali pia alikuwa ni mtu aliyekuwa akipenda kujumuika na jamii katika masuala mbali mbali ya kimaendeleo, kijamii na kiuchumi.

Akithibitisha mchango wake Marehemu huyo katika harakati za kisiasa ndani na nje ya Naibu Katibu Mkuu Mstaafu, Vuai Ali Vuai Alieleza kwamba Hamdani alikuwa ni mtu makini na mkweli katika utumishi wake na aliyetamani mabadiliko ya kimaendeleo katika sehemu yake ya kazi na chama kwa ujumla.

Mara baada ya maziko hayo palisomwa wasifu wa marehemu Hamdani kuwa alizaliwa mwaka 1963, huko Donge.
Amewahi kushika nafasi mbali mbali za uongozi na utendaji ndani ya chama na jumuiya zake baada ya kujiunga na CCM mwaka 1987 ambapo mwaka 1988 alikuwa katibu wa UVCCM Tawi la Donge Mtambile mwaka, Katibu wa UVCCM Wilaya ya Kusini hadi kufikiwa na mauti alikuwa ni Katibu wa CCM Wilaya ya  Kusini Unguja.

Mwenyezi mungu amlaze mahali pema peponi Amin.
Share on Google Plus

0 comments: