SIASA za nchi kadri ya muda unavyozidi kwenda ndipo kunazidi kuzaliwa kundi kubwa la wanasiasa wasiokuwa na uelewa wa mambo mengi hasa wanasiasa kutoka vyama vya upinzani, ambao muda mwingi wamekuwa si wa kweli na ni watu wanaosababisha matatizo lukuki na mpasuko kwenye jamii zetu.
Toka lilipotokea tukio baya la kushambuliwa kwa silaha kwa mbunge wa Singida Mashariki-CHADEMA, Tundu Lissu na baadaye kulazwa kwa ajili ya matibabu Nairobi, Kenya, kumeendelea kujitokeza matukio mbalimbali ambayo kwa namna moja au nyingine yamekuwa yakieneza utoto na hata kuondo ule utu wetu tuliokuwa awali.
Sitaki na sintoingilia uchunguzi unaofanywa na vyombo vya usalama lakini kubwa zaidi ambalo ninalolizungumzia ni hatua ya wabunge wa CHADEMA, akiwemo Peter Msigwa mbunge wa Iringa Mjini na Godbless Lema mbunge wa Arusha Mjini wa CHADEMA, ambao wametoa taarifa ya kulishutumu bunge na japokuwa sitaki kuamini kauli za wabunge hao zina baraka za chama hicho.
Wote tunakubaliana sote kwamba tukio lilimtokea Lissu ni ovu na lakusikitisha na linapaswa kukemewa na kila mtu, lakini tukio hili lisitumike vibaya katika kutafuta uhalali au na umaarufu wa kisiasa katika mfumo hasi, ambao utalipasua taifa bila ya kuwepo kwa sababu za msingi kwenye kuleta maendeleo kwa wananchi.
Jamii pia inapaswa kuelewa kuwa ni mpuuzi tu, ndiye atakayeweza kumbebesha spika Job Ndugai, mzigo wa lawama kutokana na kilichotokea kwa Lisu au kwa nini Bunge halikuchukua jukumu la kwenda kumtibia nje ya nchi, wakati Ndugai alishatoa mwelekeo wa nini kilichotokea ikiwemo kwa familia ya Lissu yenyewe kukataa kwa ndugu yao kutibiwa nchini.
Lazima tukubaliane kauli za Lema na Msigwa ni kauli za kipuuzi zinazopaswa kukemewa kwa nguvu kubwa na pia zieleweke kuwa kauli hizo zinatokana na wao kulelewa kwenye Chama chenye misingi ya umangimeza na ndio maana wanashindwa kumtibia mwenzao, na badala yake wapo kwenye kupiga kelele serikali haijamtibia mbunge huyo.
Ni upuuzi mkubwa kwa mbunge mwenye kundi la watu kusema kwenye mitandao ya kijamii kuwa Spika Ndugai alipaswa kulihairisha bunge kutokana na tukio hilo, lakini lazima jamii ielewe na kuelezwa katika kanuni za kudumu za bunge hakuna kipengele hata kimoja kinachoeleza kuwa mbunge akipigwa na kupelekwa hospitali bunge litasimamishwa.
Kanuni zinaeleza kuwa bunge litasimama kwa kutokea kwa msiba wa mbunge ndipo Spika atatangaza ahirisho la bunge. Sasa tujiulize hivi wabunge wanapotaka bunge lingeahirishwa au walijua kuwa Lissu atafariki dunia?. Ni utoto wa kiwango cha juu kinachoonyesha CHADEMA ni mkusanyiko wa watu wasiojielewa na ndio maana wanaruhusu watu kuzungumza ovyo.
CHADEMA walipaswa kufahamu kuwa jambo hili limefanikiwa kuwaleta watu pamoja na ndio maana Chama Cha Mapinduzi(CCM) wametoa tamko la kulaani na hata kuwa na taarifa za mara kwa mara kuhusiana na tukio hilo, ikiwemo kupongeza au kulaani pale jambo nzuri linapofanyika na wao kuzungumza.
Pia, ni jambo la ajabu kuwepo kwa kundi la wabunge hasa la upinzani linalotaka Bunge lijadili ulinzi wa wabunge pekee na sio ulinzi wa raia na mali zao, hasa wakati huu ambao kiongozi wa serikali bungeni, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, ameshatoa maelekezo kuwa nchi iko salama na hakuna tatizo lolote la usalama.
Kauli hiyo ilitosha kuwafanya CHADEMA kuwa wamoja na kuachana na porojo zisizokuwa na sababu za msingi, ambazo zimekuwa hazileti tija kwenye mfumo sahihi wa maisha ya wananchi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakiishi kwa amani na utulivu na hakuna kuwepo kwa tishio lolote la usalama.
Spika Ndugai anapaswa kufahamu kuwa aliposhika ashikiria na asitetereke hata kidogo, kwa kuwa watanzania wazalendo wapo pamoja naye kwenye kusimamia haki na wajibu wa kila mtanzania, ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuleta mabadiliko chanya na kumpa ushirikiano yeye binafsi na rais Dk. John Magufuli.
Kwa mantiki hiyo, suala la Lissu linazidi kuwapa mwangaza watanzania kuwa CHADEMA sio Chama imara bali ni mkusanyiko wa wasakatonge wenye hulka ya umangimeza na ndio maana wamegeuza mtaji afya ya mbunge wao ili waweze kujipatia mambo mbalimbali, ambayo kwa namna moja au nyingine hayana msaada kwa taifa.
0 comments: