Chama
cha Wananchi(CUF), upande wa Profesa Ibrahim Lipumba kimesema
kitashiriki kikamilifu katika uchaguzi wa madiwani uliopangwa kufanyika
Novemba 26 lakini kimesisitiza kutoshirikiana na Ukawa.
Hii
ni mara ya kwanza kwa chama hicho kuweka msimamo wake katika uchaguzi
tangu kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo CUF ilikuwa
miongoni mwa vyama viliunda umoja huo kwa kuweka wagombea
waliokubaliana.
Mkurugenzi
wa Habari na Uenezi wa CUF, Abdul Kambaya amesema jana Jumamosi jijini
kuwa chama hicho hakioni sababu yoyote ya kushirikiana na vyama vingine
kwenye uchaguzi huo ambao unahusisha halmashauri 34.
“CUF
tunashiriki kwenye uchaguzi huu lakini hatututegemei kushirikiana na
umoja wowote ule, sisi hatuitambui Ukawa lakini tunajua kuna chama kama
Chadema, CUF na vyama vingine,” alisema Kambaya wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za chama hicho zilizopo
Buguruni.
Alisema
chama hicho kimejipanga vilivyo kuelekea kwenye uchaguzi huo na kwamba
ili kuwaletea maendeleo wananchi wa maeneo hayo kunahitajika kuwa na
viongozi wenye utulivu wa akili.
“Sisi tuko tayari kuelekea kwenye uchaguzi huo bila kuhusishwa na chama kingine chochote tunaamini tutafanya vizuri,” alisema.
Awali,
mkurugenzi wa uchaguzi wa chama hicho, Jafari Mneko aliwataka wana CUF
kujitokeza kwa wingi katika kinyang’anyiro hicho. Amesema chama chake
kimepokea taarifa kutoka ofisi ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiwaarifu
kuhusu uchaguzi huo.
“Tumepata
barua kutoka tume ambayo imetueleza kuhusu tarehe ya kufanyika kwa
uchaguzi huo na sisi tumeanza kujiandaa na ndiyo maana tunawaomba
wanachama wetu wanaohisi wana uwezo wajitokeze kuomba nafasi na baadaye
viongozi wa chama watachuja majina yao,” alisema.
Katika
hatua nyingine mkurugenzi huyo alionya kile alichokiita mali ya chama
kutumika kinyume na sheria na akawataka wanachama kutetea maslahi ya
chama chao.
“Kuanzia
sasa hatutapenda kuona mali ya chama kama mihuri, bendera ikiendelea
kuchezewa ovyo, tunawataka wanachama kuzingatia katiba ya chama ibara ya
12 ambayo inamtaka kila mwanachama kulinda katiba na imani ya chama,”
alisema.
0 comments: