IGP SIRRO AZUNGUMZIA KUHUSU MIILI YA WATU ILIYOOKOTWA BAHARINI
Inspekta
Jenerali wa Polisi, Simon Sirro amesema wameunda timu ya wataalamu
kuchunguza miili iliyookotwa na sampuli kutoka miili hiyo zimechukuliwa.
Amesema iwapo kuna watu ambao ndugu zao wamepotea ni vyema wakafika
katika ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kwa
ajili ya vipimo na kufanyika upelelezi.
“Bahari ni kubwa inapita katika nchi nyingi na inachukua kila kitu, haya
mambo yanapotokea hata nchi nyingine yanatokea, kwa hiyo kimsingi
tumeunda timu ya wataalamu ya kupeleleza kuhusu miili hii, wamechukua
majimaji kutoka mwilini,” alisema.
IGP Sirro alisema, “Kama kuna mtu ambaye ndugu yake amepotea afike makao
makuu ya Polisi upande wa DCI tuweze kufanya uchunguzi kuona kama ni
ndugu yake.”
Alisema miili hiyo haijabainika kuwa ni ya watu wa Taifa gani.
“Tatizo letu Watanzania ni kwamba moja kwa moja wanaanza kuhisi, sijui
kwa nini tunakuwa tunaishi kwa hisia na hii hisia hisia si nzuri, tuseme
kitu tukiwa na uhakika. Ikitokea jambo utasema ni Sirro, utasema ni
nani, hii si nzuri na niwaambie tumwogope Mungu pia,” alisema IGP SIRRO
0 comments: