Kila mkuu wa mkoa nchini ameagizwa kujenga viwanda vipya 100 katika kipindi cha mwaka mmoja kinachoanzia Desemba 2017.
Akizungumza
na wakuu wa mikoa wapya walioapishwa juzi Ikulu jijini Dar es Salaam,
waziri wa nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(Tamisemi), Selemani Jafo aliwataka kuitekeleza ipasavyo sera ya ujenzi
wa viwanda.
Jafo
alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa ifikapo Desemba 2018 kila
mkoa uwe umejenga viwanda vidogo na vya kati visivyopungua 100.
Alisema
mikoa 26 ya Tanzania Bara inatakiwa kuwa na viwanda vipya vidogo na vya
kati visivyopungua 2,600 ifikapo Desemba 2018. Alisema Serikali
imekusudia kufikia nchi ya uchumi wa kati kupitia ujenzi wa viwanda huku
akiwataka wakuu hao kuibua viwanda vidogo na vya kati kwa kuhamasisha
ushiriki wa viongozi ndani ya mikoa na wananchi katika maeneo yao ya
utawala.
Jafo
aliongeza kuwa, katika kusimamia utekelezaji wa agizo hilo ofisi yake
itaweka utaratibu maalumu wa kupima utendaji kazi wa kila kiongozi wa
mkoa kwa kuangalia ushiriki wake wa kuwajengea hamasa viongozi wa chini
wakiwamo wakuu wa wilaya na wananchi.
Alisema
katika kufanikisha dhana ya ujenzi wa uchumi wa viwanda, Serikali
inaendelea kuweka mkazo na kipaumbele katika upatikanaji wa malighafi za
kilimo na kuwataka wakuu wa mikoa kuhakikisha kuwa maofisa ugani
wanatekeleza vyema majukumu yao ya kazi.
Pia,
aliwataka wakuu hao wa mikoa kusimamia makusanyo ya fedha za ndani
katika halmashauri na kutumia vyema asilimia tano zinazotengwa
kuwawezesha wananchi kupata mikopo ili washiriki katika ujenzi wa uchumi
wa viwanda.
Mkuu
wa Mkoa wa Mara, Adam Malima alisema ili kufanikisha dhana ya uchumi wa
viwanda, Serikali haina budi kuwapa msukumo na ushirikiano wa karibu
wanasayansi utakaowezesha kuibua viwanda vingi zaidi pamoja na
kuhakikisha upatikanaji wa malighafi za kilimo nchini.
Mbali
na Malima, wakuu wengine wa mikoa waliohudhuria mkutano huo ni Robert
Luhumbi (Geita), Joachim Wangabo (Rukwa), Galesius Byakanwa (Mtwara) na
Christine Mndeme (Ruvuma).
0 comments: