Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda amesema serikali inaendelea na
jitihada za kurekebisha miundombinu iliyoharibiwa na mvua, zilizonyesha
hivi karibuni ili wananchi waendelee na shughuli za kiuchumi.
Aidha,
Makonda amesema Benki ya Dunia imetoa Sh bilioni moja kwa ajili ya
kusafisha eneo la Jangwani, bonde la Mto Msimbazi na kazi ya usafishaji
inatarajiwa kuanza wiki ijayo baada ya kukamilisha hatua za kumpata
mkandarasi.
Makonda
alisema hayo jana wakati wa ziara ya kukagua athari, zilizosababishwa
na mvua hizo katika maeneo mbalimbali ya jiji na kuliagiza Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kujenga daraja la muda katika eneo la Mbezi
Beach Daraja la Malecela, lililoharibika kutokana na mvua hizo.
“Wakati
Tanroads wanaendelea kurejesha miundombinu katika hali ya kawaida,
Jeshi letu la (JWTZ) litatusaidia kujenga daraja la muda ili kuhakikisha
watu wanapita na kuendelea na shughuli zao, niwaombe tu muwape
ushirikiano wakati wakifanya kazi hiyo na mimi naamini watafanya haraka
na itapitika muda mchache,” alisema wakati akiongea na wananchi wa
maeneo hayo.
Aidha,
Makonda alisema mbali na barabara na madaraja, pia wahusika wa umeme na
maji, wanaendelea na jitihada ili kuhakikisha miundombinu hiyo inarejea
na wananchi kuendelea kupata huduma hizo muhimu.
Hata
hivyo, Makonda aliwataka watu wanaoishi katika maeneo hatarishi,
kuondoka katika maeneo hayo ili kujiepusha na hatari wanazoweza
kuzipata, kwa kuwa mvua hizo bado zinaendelea kwa mujibu wa Mamlaka ya
Hali ya Hewa (TMA).
Pia
Makonda aliwataka wananchi wenye tabia za kuchimba michanga kwenye
mito, kuacha kwa kuwa kitendo hicho kwani kinachangia uharibifu
mazingira, ambayo yanawaadhibu sasa.
“Serikali
inapotoa rai, siyo kwamba inawachukia inawatakia mema, niwaombe tena
leo kwa unyenyekevu tuchukue tahadhari, ni kwa faida yako na familia
yako, kuna baadhi tumeziba mito wengine wamefanya dampo na wengine
kuchimba mchanga, jambo ambalo linaongeza madhara kuwa makubwa,
ningeomba tu muwe mnatii tahadhari zinazotolewa na serikali,” alisema
Makonda.
Alisema
kwa Manispaa ya Kinondoni pekee, kuna nyumba 200 ambazo zipo kwenye
maeneo hatarishi huku nyumba 190 zikiwa zimebomoka, hivyo ni vyema
wananchi hao wakaendelea kuchukua tahadhari ili kuepusha madhara zaidi.
0 comments: