MZEE Joseph Sahani (60) ambaye amefariki
duniani akiwa kwa mganga wa kienyeji akifanyiwa dawa ya kuongeza nguvu
za kiume, imebainika kwamba alikuwa na wake wawili, watoto zaidi ya 10
na ameacha utajiri wa ng’ombe zaidi ya 50.
Mwili wa Mzee Sahani aliyefariki dunia
Jumapili jioni umezikwa katika Kijiji cha Ipango jirani na Kijiji cha
Nzoza mahali alipozaliwa katika Kata ya Salawe Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga mkoani Shinyanga. Alifariki dunia akiwa anapatiwa matibabu kwa
mganga wa kienyeji, Robert Mkoma ambaye anaishi wilayani Kwimba mkoani
Mwanza.
Baadhi ya wakazi wa Kijiji cha Nzoza,
Shija Kulwa na Mariamu Kuhenge walimueleza mwandishi wa habari hizi kuwa
mganga huyo siyo mkazi wa kijiji hicho, bali hutembelea maeneo
mbalimbali kwa madhumuni ya kutafuta wateja na kuwapatia huduma ya
matibabu.
Kulwa alisema Sahani alipewa taarifa na
rafiki yake, Pastori Sitta ambaye alimkaribisha mganga huyo ili afanye
matibabu kwa wenye matatizo ya kuishiwa nguvu za kiume na siyo mara yake
ya kwanza kufika katika kijiji hicho.
“Mganga huyu siyo mara yake ya kwanza
kufika katika kijiji hiki kwani alikwisha kuja na kumtibu mwanaume mmoja
aliyeishiwa nguvu za kiume na kuanza kujisifia mitaani kuwa amepona,
ndio Mzee Sita alipomfuata Mzee Sahani baada ya kuwa alimueleza naye ana
tatizo la kukosa nguvu za kiume na kumhakikishia mganga huyo anaweza
kumtibu vizuri tatizo lake,” alidai mkazi huyo wa Nzoza.
Kaimu Mwenyekiti wa Kijiji cha Nzoza,
Masalu Msalaba alisema alipewa taarifa na baadhi ya wananchi kuhusu kifo
cha Mzee Sahani, kwamba alikuwa akipatiwa matibabu kwa mganga wa
kienyeji ndipo alipochukua hatua ya kuwapigia askari Polisi wa Kituo cha
Salawe.
Diwani wa Kata ya Salawe, Joseph Buyugu
alisema mganga huyo alifika kwa mara ya kwanza kwenye familia ya Mzee
Sitta na kumtibu mwanawe aliyekuwa akidaiwa ana tatizo la kukosa nguvu
za kiume na alimtibu huku watu wakiamini alimponyesha baada ya yeye na
mkewe kukaa miaka mingi bila kupata mtoto na hatimaye akapata mtoto.
“Mganga huyo ameonekana kuaminika na
baadhi ya wananchi wa vijiji vya kata hii baada ya kusikia amerudi tena
katika familia hiyo akitokea kwenye mji wake Kwimba mkoani Mwanza kwa
lengo la kudai deni lake la uponyaji baadhi ya watu walielezana kuwa
mganga yupo na huyo mzee kujitokeza kwa kushawishika kuwa atapona
matokeo yake kupoteza maisha,” alieleza diwani Buyugu. Mzee Sahani
alifariki kwa mganga wa kienyeji Mkoma wakati akipatiwa matibabu ya
kupata nguvu za kiume kwa kuwekewa dawa aina ya unga sehemu za siri
iliyoingizwa kwa kutumia pampu ya baiskeli.
0 comments: