Milima ya Morogoro
***
MWANAFUNZI wa Chuo Kikuu cha Kiislamu
Morogoro (MUM), Victor Ibrahim (22), amefariki dunia wakati akitalii
kwenye milima baada ya kuteleza na kuangukia kwenye korongo.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Morogoro, Leonce Rwegasira, alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea
Oktoba 3, mwaka huu, majira ya jioni, katika eneo lenye milima ambalo
liko Kata ya Milimani mkoani humo.
Alisema mwanafunzi huyo akiwa na wenzake
kwenye hiyo milima, walikuwa wanafanya utalii wa ndani na ndipo
alipokanyaga eneo lenye unyevu lililoko kando ya korongo hilo refu na
kuangukia kwenye mawe.
Kamanda Rwegasira alisema juhudi za
kuutoa mwili wa kijana huyo zilifanikishwa kwa ushirikiano baina ya
kikosi cha zimamoto na polisi.
Alisema baada ya uchunguzi kufanyika, polisi waliukabidhi mwili huo kwa familia kwa ajili ya kuendelea na taratibu za mazishi.
Aidha, Kamanda alitoa wito kwa wananchi
kuwa wanapotaka kutembelea maeneo kama hayo wahakikishe wanakuwa na watu
wa kuwaongoza kwa kuwa wanafahamu sehemu hiyo ili waonyeshwe njia
ambazo ni salama.
0 comments: