Na.Jacquiline Mrisho – MAELEZO.
Serikali
imetoa onyo kali kwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Mjini, Mh. Zitto Kabwe
juu ya taarifa za upotoshaji wa takwimu za Pato la Taifa alizozitoa hivi
karibuni.
Taarifa
hizo za Mh. Zitto zimeripoti kuwa ukuaji wa Pato la Taifa kwa robo ya
pili ya mwaka 2017 kuwa ni asilimia 5.7 badala ya asilimia 7.8. Kasi ya
ukuaji ya asilimia 5.7 ilikuwa ni kwa robo ya kwanza ya Januari hadi
Machi 2017.
Onyo
hilo limetolewa jana Jijini Dar es Salaam na Bw. Daniel Masolwa Meneja
wa Takwimu za Pato la Taifa kutoka Ofisi ya Taifa za Takwimu (NBS),kwa
niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa NBS,pamoja na Mkurugenzi wa Sera na Tafiti
za Uchumi wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw.Johnson Nyella wakati
wakizungumza na Waandishi wa Habari.
Masolwa
alisema kuwa upotoshaji huo uliofanywa na Mh. Zitto ni wa makusudi na
unalenga kuonesha kuwa juhudi znazofanywa na Serikali ya Awamu ya Tano
hazina manufaa kwa Wananchi.
“Napenda
kukanusha kauli ya Mh. Zitto kuhusu taarifa zake zinazodai kuwa takwimu
za Pato la Taifa zimepikwa, Mh. Zitto anatakiwa kujua kwamba kazi ya
kukokotoa takwimu za Pato la Taifa ni ya kitaalam na inafuata miongozo
inayotolewa na Kamisheni ya Umoja wa Mataifa ya Takwimu na Shirika la
Fedha Duniani (IMF)”,alisema Masolwa.
Aliongeza
kuwa miongozo hiyo ni pamoja na mifumo ya pato la Taifa ya mwaka 2003
na 2008 na mwongozo wa kuainisha shughuli za kiuchumi Toleo la Nne
ambapo kwa mujibu wa ripoti ya Benki ya Dunia ya mwaka 2016 Tanzania
imekuwa nchi ya pili kwa nchi za kusini mwa jangwa la Sahara kwa utoaji,
uchambuzi, usimamizi na usambazaji wa takwimu kwa kipindi cha miaka
kumi iliyopita.
Aidha
Bw.Masolwa alitoa wito kwa taasisi yoyote ile au mtu binafsi anayetaka
kutayarisha takwimu rasmi kwa ajili ya kutunga sera na kupanga mipango
ya maendeleo kupata maelezo ya kina kuhusu ukokotoaji na miongozo
mbalimbali.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Sera na Tafiti za Uchumi wa Benki Kuu ya
Tanzania, Johnson Nyella alisema kuwa Mh. Zitto amekokotoa ukuaji wa
Pato la Taifa anaodai kuwa ni sahihi kwa kuangalia tofauti kati ya
ongezeko la ujazi wa fedha na mfumuko wa bei jambo ambalo sio sahihi
kulitumia kama kipimo.
“Ukokotoaji
wa aina hiyo umejengwa juu ya nadharia inayoitwa ‘quantity theory of
money’ ambayo inasema mfumuko wa bei hutokea pale fedha zinapoongezeka
kwa kasi zaidi kuliko uzalishaji wa vitu halisi ambayo si sahihi kutumia
nadharia hiyo kuelezea mfumuko wa bei na ukuaji wa uchumi katika
kipindi cha muda mfupi kama Mh. Zitto alivyofanya,” alifafanua
Bw.Nyella.
Wawakilishi
hao wa Benki Kuu na Ofisi ya Taifa ya Takwimu wamelazimika kutoa
ufafanuzi huo baada ya taarifa za Ukuaji wa Pato la taifa kutolewa na
Mh.Zito, na wakawaasa Wananchi na wanasiasa kuacha kupotosha takwimu za
serikali na kuziomba mamlaka husika kuchukua hatua kwa yeyote
atakayebainika kupotosha umma kwa makusudi.
0 comments: